16. Msingi wa tano: Ubainifu wa Allaah juu ya ni kina nani mawalii wa Allaah na wasiokuwa wao

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Msingi wa tano:

Kubainisha kwa Allaah (Subhaanah) mawalii wa Allaah na kutofautisha baina yao na wale wenye kujifananisha na wao miongoni mwa maadui wa Allaah katika wanafiki na watu waovu. Inatosha katika hili Aayah moja katika Suurah “Aal ´Imraan” ambayo ni maneno Yake:

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni. Atakupendeni Allaah na atakusameheni dhambi zenu. Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (03:31)

MAELEZO

Kubainisha kwa Allaah (Subhaanah) mawalii wa Allaah… – Huu ni msingi mkubwa kabisa. Nao ni kutenganisha kati ya mawalii wa Allaah na mawalii wa shaytwaan. Watu wa batili wamekuwa sasa wakiwaita mawalii wa shaytwaan kuwa ni mawalii wa Allaah kiasi cha kwamba jambo hili limekuwa likiwatatiza watu. Kwa ajili hii ndio maana Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ametunga kitabu chenye manufaa na chenye kufidisha kwa jina “al-Furqaan bayn Awliyaa´-ir-Rahmaan wa Awliyaa´-ish-Shaytwaan”. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika.” (10:62)

Kisha akaweka wazi zaidi kwa kusema:

الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Ambao wameamini na wakawa wachaji.” (10:63)

Hawa ndio mawalii wa Allaah. Wamekusanya kati ya imani na kumcha Allaah, elimu yenye manufaa na matendo mema. Hawa ndio mawalii wa Allaah. Mawalii wa Allaah sio wale waliotoka nje ya Shari´ah ya Allaah, wakabadilisha dini ya Allaah na wakaita katika kuabudia makaburi. Hawa ni mawalii wa shaytwaan. Walii sio mchawi, kuhani na khurafi ambaye anawaonyesha watu mambo yasiyokuwa ya kawaida ya kichawi na kudai kuwa eti ni makarama. Ukweli wa mambo ni kwamba ni mambo ya ki-Shaytwaan yenye kwenda kinyume na desturi.

Inatosha katika hili Aayah moja katika Suurah “Aal ´Imraan” – Kumpenda Allaah ni miongoni mwa aina kubwa za ´ibaadah. Alama ya kumpenda Allaah ni pamoja na kumfata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Asiyemfata Mtume huyo sio walii wa Allaah na wala hampendi Allaah. Wapotevu hawa wanapinga na kusema mtu hawi walii wa Allaah mpaka kwanza atoke nje ya utiifu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)! Walii kwa mujibu wao ni yule mwenye kutoka nje ya Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na badala yake akawa anategemea mambo ya kikhurafi na Bid´ah. Mtu kama huyu ndiye walii kwao. Wao wanasema kuwa wanamuabudu Allaah kwa sababu wanampenda na si kwamba wanamwabudu kwa kuogopa Moto Wake na kutamani Pepo Yake! Wanasema kuwa wanamuabudu kwa kuwa wanampenda tu! Nyinyi mnampenda kwa mujibu wa mfumo wa nani? Je, mnampenda kwa mujibu wa mfumo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au ni kwa mujibu wa mfumo wa mtu mwingine? Hakuna anayempenda Allaah isipokuwa yule mwenye kumfata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hiki ndio kipambanuzi kati ya walii wa Allaah na walii wa shaytwaan.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 19/05/2021