15. Namna ambavyo elimu ya Kishari´ah imekuwa ni kitu kisichojulikana kwa watu wengi

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Kisha ikawa jambo hili ni katika mambo mageni zaidi na ikawa elimu na Fiqh ndio Bid´ah na upotevu na bora walilo nalo wao ni kuchanganya haki na batili. Ikawa elimu ambayo Allaah (Ta´ala) ameifaradhisha juu ya viumbe na akaisifia hakuna mwenye kuitamka isipokuwa zindiki na mwendawazimu. Na akawa yule mwenye kuipinga na kuifanyia uadui na akaandika kutahadharisha na kukataza [juu ya mtu wa elimu] ndio msomi na mwanachuoni.

MAELEZO

Kisha ikawa jambo hili ni katika mambo mageni zaidi… – Ikawa elimu na Fiqh kwa baadhi ya wale waliokuja nyuma ndio Bid´ah na upotevu. Hili ni kwa sababu wameacha elimu sahihi iliyojengwa juu ya Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Elimu kwao ikawa ni ´fulani amesema`, ´fulani amesema` na simbulizi. Kwa mfano wanaposema kuwa kaburi fulani linanufaisha na kitu kadhaa, kuna mtu ameona usingizini maeneo fulani kuna kadhaa n.k. Hii ndio elimu ya watu hawa. Au angalau watatafuta Hadiyth zilizoundwa ambazo wanazuoni wamezifukia na kubainisha kuwa ni za uongo ambapo wapotevu wanazifanya kuwa ni Swahiyh na kuzipambia mlolongo wa wapoezi wake na hivyo wanazipitisha na kusema “Hadiyth hii ni Swahiyh”. Upande mwingine wanaacha Hadiyth ambazo ni Swahiyh zilizopokelewa na al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa´iy, Ibn Maajah na zilizo na cheni za wapokezi zinazozingatiwa. Wanaziacha hizi kwa kuwa haziafikiani nao.

Na bora walilo nalo wao ni kuchanganya haki na batili – Ni lazima kutenganisha haki na batili na kupambanua kati ya viwili hivyo. Hayo mawili yakichanganywa ni kutatiza, kufanya ghushi na kutaka kuwatia watu mchanga wa machoni.

Ikawa elimu ambayo Allaah (Ta´ala) ameifaradhisha juu ya viumbe… – Kwa sababu yanaenda kinyume na yale wanayofanya. Elimu ambayo Allaah amewasifia wenye nayo na akawatapa kwayo ikawa ndio ujinga na yule mwenye kuitamka ndio mwendawazimu kwa sababu elimu ambayo Allaah ameifaradhisha inabadilisha mambo ya watu na inabadili mila za mababa na mababu zetu!

Na akawa yule mwenye kuipinga na kuifanyia uadui… – Yule mwenye kuandika hali ya  kutahadharisha juu ya elimu yenye manufaa na badala yake akasifu elimu yenye kusimangwa na kuieneza kwa watu akawa ndio msomi na mwanachuoni. Ama kuhusu yule mwenye kueneza elimu sahihi wanasema kuwa hafai na kwamba ni mjinga, anataka kuwatenganisha watu na kwamba wao wanachotaka ni kuwafanya watu wawe na umoja na si kuleta mfarakano. Ina maana mnataka kuwakusanya watu hata kama umoja huo utakuwa juu ya batili na hamtaki ufarikisho wenye kutenganisha kati ya haki na batili, kizuri na kibaya? Hili ni jambo lisilowezekana kabisa. Haiwezekani kupatikana umoja juu ya batili. Umoja unakuwa juu ya haki. Mshairi anasema:

Pale ambapo donda huzidi kuharibika

basi hapo ndipo hubainika kuzembea kwa daktari

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 33-34
  • Imechapishwa: 19/05/2021