17. Mlinganizi awe na maneno laini na asubiri

Ni lazima kwa anayelingania kwa Allaah (´Azza wa Jall) afanye hivo kwa hekima, aanze kwayo na aipatilize. Akiwa yule mwenye kulinganiwa yuko na baadhi ya ususuwavu na upinzani, basi atamlingania kwa maneno mazuri na kwa Aayah na Hadiyth zenye mawaidha na kuvutia. Akiwa na hoja tata basi atajadiliana naye kwa njia iliyo bora zaidi na asimfanyie ukali. Bali amsubirie na wala asifanye haraka na ukali. Bali ajitahidi kumfichulia hoja tata na kumuwekea wazi dalili kwa njia nzuri. Namna hii, ee mlinganizi, unatakiwa kuvumilia, kusubiri na wala usifanye ugumu. Kufanya hivo kuko karibu zaidi na kunufaika na haki, kuikubali, kuathirika yule mlinganiwa na kusubiri yale majadiliano na mahojiano.

Allaah alimwamrisha Muusa na Haruun wakati alipowatuma kwa Fir´awn wamwambie maneno laini ilihali ni mchupaji mpaka mkubwa. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amemwambia Muusa na Haaruun:

فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَّيِّنًا لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَىٰ

“Mwambieni maneno laini huenda akawaidhika au akaogopa.”[1]

Allaah (Subhaanah) amesema kumwambia Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ

”Basi ni kwa rehema kutoka kwa Allaah umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangelikukimbia.”[2]

Kwa hivyo ikatambulika kwa mambo hayo kwamba njia ya hekima na ilionyooka  katika kulingania ni kwamba mlinganizi awe mwenye hekima katika ulinganizi na mtambuzi wa njia yake. Asifanye haraka na wala asifanye ususuwavu. Bali alinganie kwa hekima. Ni yale maneno ya wazi yanayoisibu haki katika Aayah na Hadiyth na kwa mawaidha mazuri na kujadiliana kwa njia iliyo bora zaidi. Hii ndio njia ambayo unatakiwa kushika wakati wa kulingania kwako kwa Allaah (´Azza wa Jall).

[1] 20:44

[2] 03:159

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 12/06/2023