16. Mlinganizi awe na hekima na maneno mazuri

2 – Namna ya kuifanya na njia zake

Allaah (´Azza wa Jall) amebainisha namna na njia za kulingania ndani ya Kitabu Chake kitukufu na ndani ya yale yaliyokuja katika Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Miongoni mwa dalili zilizo wazi zaidi ni maneno Yake (Jalla wa ´Alaa):

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[1]

Ameweka wazi (Subhaanah) namna ambayo mlinganizi anapasa kusifika nayo na kufuata. Anatakiwa kuanza ulinganizi wake kwa hekima. Makusudio ni zile dalili za kukinaisha, za wazi na zinazofichua haki na zinazoteketeza batili. Kwa ajili hiyo baadhi ya wafasiri wa Qur-aan wamesema maana yake ni kwa Qur-aan. Qur-aan ndio hekima kubwa. Ndani yake mna ubainifu na kuiweka wazi haki kwa njia kamilifu zaidi. Baadhi ya wengine wamesema kuwa maana yake ni kwa dalili za Qur-aan na Sunnah.

Kwa hali yoyote hekima ni neno kubwa. Maana yake ni kulingania kwa Allaah kwa elimu na utambuzi na kwa dalili za wazi, zenye kukinaisha na zinazoiweka wazi ile haki na kuibainisha. Ni neno shirikishi ambalo husemwa kwa kuachiwa na kukakusudiwa maana nyingi. Husemwa kwa kuachiwa na kukakusudiwa utume, elimu na kuwa na ufahamu katika dini, akili, uchaji na mambo mengine. Msingi wa neno hilo, kama alivosema ash-Shawkaaniy (Rahimahu Allaah):

“Jambo linalozuia kutokana na upumbavu.”[2]

Hii ndio hekima.

Maana yake ni kila neno na kila kauli inayokuzuilia kutokana na upumbavu na kumkemea kutokamana na batili. Hiyo ndio hekima. Vivyo hivyo maneno yote yaliyo wazi na sahihi kwa dhati yake ndio hekima. Aayah za Qur-aan zina haki zaidi ya kuitwa hekima. Vilevile Sunnah Swahiyh zina haki zaidi ya kuitwa hekima baada ya Qur-aan. Allaah ameita Sunnah kuwa ni hekima ndani ya Kitabu Chake kitukufu. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ

”… anawafunza Kitabu na hekima… ”[3]

Bi maana Sunnah.

 Vilevile amesema (Subhaanah):

يُؤْتِي الْحِكْمَةَ مَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُؤْتَ الْحِكْمَةَ فَقَدْ أُوتِيَ خَيْرًا كَثِيرًا

“Humpa hekima Amtakaye na anayepewa hekima basi kwa hakika amepewa kheri nyingi.”[4]

Dalili za wazi zinaitwa hekima. Maneno ya wazi yanayolenga haki yanaitwa hekima kama tulivyotangulia kutaja. Miongoni mwa hayo ni chuma (الحكمة) kinachokuwa mdomoni mwa farasi. Chuma hicho kimeitwa hivyo kwa sababu kinamzuia farasi kusonga mbele mwenye nayo akikivuta kwa chuma hichi. Hekima ni neno linalomzuia anayelisikia kuendelea katika batili na linamwita kuishika haki na kushawishika nayo na kusimama kwenye mpaka uliyowekwa na Allaah (´Azza wa Jall).

[1] 16:125

[2] Fath-ul-Qadiyr (01/438).

[3] 02:129

[4] 02:269

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 25-27
  • Imechapishwa: 12/06/2023