Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Imaam Abu ´Abdillaah Ahmad bin Muhammad bin Hanbal (Radhiya Allaahu ´anh) amesema kuhusu maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah anashuka katika mbingu ya chini.”[1]

“Hakika Allaah ataonekana Qiyaamah.”[2]

na Hadiyth nyinginezo mfano wake”, tunaziamini na tunazisadikisha pasi na namna wala maana[3]. Haturudishi kitu katika hayo. Tunatambua kwamba yale yote yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni ya kweli midhali yana isinadi zilizo Swahiyh. Haturudishi neno hata moja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) hasifiwi zaidi kuliko vile alivyojisifu Yeye Mwenyewe au alivyomsifu Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), pasi na kikomo wala kiwango:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

 “Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”

Tunasema kama alivyosema na tunamsifu kama alivyojisifia Mwenyewe – hatuvuki hayo. Wenye kusifu hawawezi kufikia sifa Zake. Tunaiamini Qur-aan yote; zile Aayah zilizo wazi na zile Aayah zisizokuwa wazi. Hatumwondoshei kitu katika sifa Zake kwa sababu ya matusi. Hatuvuki Qur-aan na Hadiyth na wala hatutambui namna gani zimekuwa hivyo isipokuwa kwa kumsadikisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuthibitisha Qur-aan[4].

MAELEZO

Yaliyomo ndani ya maneno ya Imaam Ahmad kuhusu Hadiyth za kushuka kwa Allaah na mfano wake.

Maneno ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ambayo ameyanukuu mtunzi wa kitabu yamekusanya yafuatayo:

1 – Ulazima wa kuamini na kusadikisha zile Hadiyth kuhusu sifa za Allaah zilizopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kuzidisha, kupunguza wala kikomo wala kiwango.

2 – Hakuna namna wala maana bi maana hatuzifanyii namna sifa hizi. Kwa sababu kuzifanyia namna kunapingana na yale yaliyokwishatangulia. Makusudio yake si kwamba sifa Zake hazina namna. Kwani sifa Zake zimethibiti kikweli. Kila kitu kilichothibiti basi ni lazima kiwe na namna. Lakini sisi hatutambui namna zilivyo sifa za Allaah. Maneno yake aliposema:

“… wala maana.”

ni kwamba hatuzithibitishii maana inayoenda kinyume na udhahiri wake kama walivofanya Ahl-ut-Ta´wiyl. Makusudio sio kupinga maana sahihi inayoafikiana na udhahiri wake ambao umefasiriwa na Salaf. Haya yamethibiti. Haya yanafahamishwa na pale aliposema:

“Haturudishi chochote katika sifa Zake na tunamsifu kama alivyojisifu Mwenyewe na wala hatumwondoshei sifa yoyote miongoni mwa sifa Zake kwa sababu ya matusi na wala hatujui wala hatutambui namna gani zimekuwa hivyo.”

Kupinga kwake kurudisha nyuma yoyote katika sifa Zake na kupinga kujua namna Yake ni dalili ya kuzithibitishia maana iliyokusudiwa nazo.

3 – Ulazima wa kuiamini Qur-aan yote; zile Aayah ambazo maana yake iko wazi na zile Aayah ambazo maana yake haiko wazi. Tunatakiwa kurudisha zile Aayah ambazo maana yake inatatiza katika zile Aayah ambazo maana yake iko wazi ili maana yake ibainike. Maana yake isipobainika basi tunalazimika kuziamini kimatamshi na kutegemeza maana yake kwa Allaah (Ta´ala).

[1] al-Bukhaariy (1145), (6321) na (7494) na Muslim (758).

[2] Muslim (181).

[3] Maana aliyoikanusha Imaam Ahmad katika maneno yake ni ile maana iliyozushwa na Mu´attwilah katika Jahmiyyah na wengineo na wanageuza maandiko ya Qur-aan na Sunnah kutoka katika uinje wake na kupeleka katika maana inayoenda kinyume navyo. Kinachojulisha yale tuliyoyataja ni kwamba amekataa maana na amekataa namna ili maneno yake yakusanye radd kwa mapote yote mawili yaliyozuliwa; pote la Mu´attwilah na pote la Mushabbihah. (Fath-ur-Rabb al-Bariyyah, uk. 63).

[4] Tazama ”Manaaqib al-Imaam Ahmad”, uk. 156 ya Imaam Ibn-ul-Jawziy, ”Taariykh-ul-Islaam”, uk. 27 ya Imaam adh-Dhahabiy, ”Mukhtaswar as-Sawaa´iq al-Mursalah” (2(251) ya Imaam Ibn Muusuliy na ”´Ibtwaal at-Ta´wiylaat li Akhbaar-is-Swifaat” (1/44-45) ya Imaam Abu Ya´la.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 34-36
  • Imechapishwa: 13/10/2022