17. Imaam Idriys ash-Shaafi´iy kuhusu sifa za Allaah

Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Imaam Abu ´Abdillaah Muhammad bin Idriys ash-Shaafi’iy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nimemuamini Allaah na yaliyokuja kutoka kwa Allaah kama alivyokusudia Allaah. Vilevile nimemuamini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yaliyokuja kutoka kwa Mtume wa Allaah kama alivyokusudia Mtume wa Allaah.”[1]

MAELEZO

Yaliyomo ndani ya maneno ya Imaam ash-Shaafi´iy

Maneno ya Imaam ash-Shaafi´iy yamekusanya yafuatayo:

1 – Kuyaamini yale yaliyokuja kutoka kwa Allaah (Ta´ala) katika Kitabu Chake kinachobainisha kwa mujibu wa vile alivyotaka Allaah pasi na kuzidisha, kupunguza wala kupotosha.

2 – Kuyaamini yale yaliyokuja kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mujibu wa vile alivyotaka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kuzidisha, kupunguza wala kupotosha.

Maneno haya yanawarudi Ahl-ut-Ta´wiyl na Ahl-ut-Tamthiyl. Wote wawili hawajaamini yaliyokuja kutoka kwa Allaah na Mtume Wake vile alivyokusudia Allaah na Mtume Wake. Ahl-ut-Ta´wiyl wamepunguza na Ahl-ut-Tamthiyl wamezidisha.

[1] Tazama ”al-Fataawaa al-Hamawiyyah al-Kubraa”, uk. 121 ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Kuhusu ambayo amesema ash-Shaafi´iy ni haki ambayo ni lazima kwa kila muumini kuiamini. Yule atakayeyaamini an asifanye kitu cha kuyatengua, basi hakika ameshika njia salama duniani na Aakhirah.”

Miongoni mwa maneno ya ash-Shaafi´iy ambayo ni muhimu katika mlango kuhusu majina na sifa za Allaah ni pale aliposema:

”Allaah (Ta´ala) anayo majina na sifa ambazo haitakikani kwa yeyote ambaye imemsimamikia hoja akazikataa. Akienda kinyume baada ya kwamba hoja imemsimamikia basi ni kafiri. Lakini kabla ya hoja kumsimamikia ni mwenye kupewa udhuru kutokana na ujinga. Kwa sababu hayo hayatambuliki kwa akili wala kwa maono na kufikiri. Anatakiwa kuzithibitisha sifa hizi na kuzikanushia ushabihisho kama alivyojikanushia Mwenyewe:

” لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (Mukhtaswar-ul-´Uluww, uk. 177 ya al-Albaaniy na ”Ijtimaa´-ul-Juyuush al-Islaamiyyah, uk. 59.)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 36-37
  • Imechapishwa: 13/10/2022