Amesema tena (Rahimahu Allaah):

”Amri ya kuafikiana na watu, au kujitofautisha nao, kunaweza kutokana na lengo la kuafikiana nao au kutofautiana nao kuna manufaa. Basi vivyo hivyo kile kitendo cha kuafikiana au kutofautiana nao kina manufaa. Kwa maana nyingine kitendo hicho kinapelekea katika manufaa au madhara kwa mja. Ikiwa kitendo hicho hakipelekei katika maafikiano au kujitofautisha hukohuko, basi kisingelipelekea katika manufaa na madhara hayo. Kwa ajili hiyo sisi tunanufaisha na kule kuyafuata kwetu matendo yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayi wa sallam) na ya wale wanamme waliotangulia endapo wasingeyafanya, kwa sababu linarithisha kuwapenda na nyoyo zetu kuungana na nyoyo zao. Hilo linatufanya kuafikiana nao katika mambo mengine na faida nyenginezo. Vivo hivyo tunadhurika kwa kule kuafikiana na matendo ya makafiri ambayo tusingedhurika iwapo tusingeliyafanya. Kitendo ambacho ni kuafikiana au kujitofautisha nao kinaweza kuwa na manufaa au madhara hata kama wao hawakukifanya. Hata hivyo kimeitwa kwenda sambamba au kujitofautisha nao kwa njia ya majulisho na utambulisho. Kwa maana hiyo kuafikiana nao inakuwa ni dalili juu ya madhara na kujitofautisha nao ni dalili juu ya manufaa. Katika hali hii kuafikiana na kujitofautisha nao inakuwa inahusiana na majulisho, ilihali ile hali ya kwanza inahusiana na sababu. Wakati fulani yanaweza kukusanyika yote mawili, nayo ni ile hekima yenyewe inayotokana na kitendo chenyewe ambacho tumeenda sambamba nao au tumejitofautisha nao au kushirikiana nao kwenyewe. Hali huwa namna hiyo mara nyingi juu ya suala la kwenda sambamba nao ambako kumekatazwa au kujitofautisha nao ambako kumeamrishwa. Ni lazima kuifahamu maana hii, kwa sababu kupitia yenyewe ndio mtu atapata kujua ni kwa nini Allaah ametukataza kuwaigiliza na kujifananisha nao kwa njia ya kuachia na iliyofungamana.”[1]

Kiungo hichi kinachounganisha kati ya yale ya nje ya na ya ndani, ni jambo lililothibitishwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). an-Nu´maan bin Bashiyr (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akizinyoosha safu zetu kana kwamba anayoosha kwazo manyayo ya mshale mpaka pale alipoona kuwa tumelielewa. Siku moja alijitokeza kwetu akasema: ”Enyi waja Allaah! Hakika mtazinyoosha safu zenu au Allaah atazitofautisha kati ya nyuso zenu.”

Imekuja katika upokezi mwingine ”nyoyo zetu”[2]. Akaashiria kuwa kujitofautisha kwa nje – ijapo inahusiana na kuzinyoosha safu peke yake – kunapelekea kutofautiana kwa nyoyo, jambo ambalo linajulisha kuwa uinje una athari juu ya yale yaliyomo ndani.

[1] Iqtidhwaa’-us-Swiraat al-Mustaqiym, uk. 7-8

[2] Muslim na Abu ´Awaanah. Upokezi mwingine ni wa Abu Daawuud. Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh. Tazama ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (668-669).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 209-210
  • Imechapishwa: 28/11/2023