15. Muislamu anaombwa katika uhai wake na si baada ya kufa kwake

Swali: Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمً فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Hatukutuma Mtume yeyote isipokuwa atiiwe kwa idhini ya Allaah. Na lau wao pale walipojidhulumu nafsi zao wangelikujia wakamuomba Allaah msamaha na Mtume akawaombea msamaha, basi wangelimkuta Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kati yao kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kwa kujisalimisha.”[1]

Wako waislamu wanaojengea dalili Aayah hii ya kwamba hapana vibaya kwa muislamu kwenda na kufunga safari kuliendea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumtaka Mtume wa Allaah amwombee msamaha ilihali yuko ndani ya kaburi lake. Je, kitendo hichi ni sahihi kama alivosema (Ta´ala)? Je, maana ya (جاءوك) ni kipindi yuko hai au baada ya kufa kwake? Je, muislamu anaritadi asipohukumiana na Sunnah ya Mtume wa Allaah? Je, inafaa kwa watu wakazozana juu ya dunia au dini?

Jibu: Aayah hii tukufu inawahimiza Ummah kumwendea yeye pindi wanapozidhulumu nafsi zao kwa kufanya kitu katika dini au wakatumbukia katika ambalo ni kubwa kuliko hilo ambalo ni shirki. Basi katika hali hiyo inawahimiza wamwendee yeye hali ya kuwa ni wenye kutubia na wenye kujuta ili aweze (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaombea msamaha. Makusudio ya ujio huu ni pindi yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko hai. Anawaita wanafiki na watu wengine wamwendee ili watangaze kutubia kwao na kurejea kwao kwa Allaah na wamwombe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awaombee kwa Allaah azikubali tawbah zao na azitengeneze hali zao. Kwa ajili hii ndio maana akasema:

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Hatukutuma Mtume yeyote isipokuwa atiiwe kwa idhini ya Allaah.”[2]

Kumtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunakuwa kwa idhini ya Allaah ambayo ni ile idhini ya kilimwengu ya ki-Qadar. Yule ambaye Allaah amemwidhinishia na akataka kuongoka kwake ataongoka, na yule asiyemwidhinishia Allaah kuongoka kwake haongoki. Jambo liko mikononi Mwake (Subhaanah). Kile anachotaka Allaah kiwe, kinakuwa, na kile ambacho Allaah hakutaka kiwe, hakiwi:

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

”Hamtotaka isipokuwa atake Allaah, Mola wa walimwengu.”[3]

Kuhusu idhini ya ki-Shari´ah amedhinisha (Subhaanah) kwa viumbe wote; majini na watu waongoke na akataka kutoka kwao ki-Shari´ah na kawaamrisha jambo hilo. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ

”Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu.”[4]

يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُبَيِّنَ لَكُمْ وَيَهْدِيَكُمْ سُنَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ وَيَتُوبَ عَلَيْكُمْ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Allaah anataka kukubainishieni na kukuongozeni nyendo za wale walio kabla yenu na apokee tawbah kwenu. Na Allaah Mjuzi, Mwenye hekima.”[5]

Kisha akasema:

وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا

“Lau wao pale walipojidhulumu nafsi zao wangelikujia wakamuomba Allaah msamaha na Mtume akawaombea msamaha, basi wangelimkuta Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu.”[6]

Hali ya kuwa ni wenye kutubia na si kwa kuzungumza peke yake:

فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ

“… wakamuomba Allaah msamaha na Mtume akawaombea msamaha… “

Bi maana akawaombea msamaha.

لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا

“… basi wangelimkuta Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu.”[7]

Ni mahimizo kwa waja wamwendee Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamtangazie mbele yake tawbah yake na awaombee kwa Allaah. Makusudio sio baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama wanavofikiria baadhi ya wajinga. Kumwendea baada ya kufa kwake kwa lengo hili si jambo limewekwa katika Shari´ah. Anamwendea kumtolea salamu yule ambaye yuko Madiynah au amemfikia kutoka nje kwa lengo la kuswali msikitini mwake, kusoma humo na kadhalika. Akifika msikitini atamtolea salamu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na marafiki zake. Lakini asifunge safari kwa ajili ya kulitembelea kaburi peke yake. Bali iwe kwa ajili ya kuutembelea msikiti. Matembezi ya kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kaburi la as-Swiddiyq na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) yatakuwa ni yenye kufuatia matembezi ya msikiti. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kusifungwe safari isipokuwa kuelekea katika misikiti mitatu; msikiti Mtakatifu, msikiti huu na msikiti wa al-Aqswaa.”[8]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Hakufungwi safari kwa ajili ya makaburi. Lakini wakati atapofika msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi itasuniwa kwake kumtolea salamu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na marafiki zake (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Lakini asifunge safari kwa ajili ya kulitembelea kaburi peke yake kutokana na Hadiyth zilizotangulia.

Ama yale yanayohusiana na kuomba msamaha inakuwa katika uhai wake na si baada ya kufa kwake. Dalili juu ya haya ni kwamba Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) hawakufanya hivo ilihali wao ni wajuzi zaidi wa kumtambua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wenye kuelewa zaidi dini yake. Isitoshe yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hamiliki jambo hilo baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[9]

Kuhusu yale aliyoeleza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya kwamba anayemswalia basi anaonyeshwa swalah ya mtu huyo, hilo ni jambo maalum linalohusu kumswalia. Ambaye anamswalia basi Allaah anamswalia mara kumi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Niswalieni kwa wingi. Kwani hakika ya swalah zenu ni zenye kuonyeshwa kwangu.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni vipi utaonyeshwa swalah zetu ili umekwishateketea?” Akasema: “Allaah ameuharamishia udongo kula miili ya Mitume.”[10]

Hili hukumu yake ni maalum kuhusu kumswalia. Katika Hadiyth nyingine amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah anao Malaika wanaozunguka ambao wanafikisha salamu kutoka kwa Ummah wangu.”[11]

Hili ni jambo maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba zinamfikia. Ama yule ambaye ameidhulumu nafsi yake kumwendea akaomba msamaha mbele ya kaburi lake ni kitu hakina msingi. Bali ni maovu na haijuzu. Aidha ni njia inayopelekea katika shirki. Kwa mfano akamwendea akamwomba uombezi, kuwaponya wagonjwa, nusura dhidi ya maadui au akamwambia amwombee ni mambo yasiyojuzu. Haya si katika mambo maalum kwake yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kufa kwake wala si katika mambo maalum kwa wengine. Kila anayekufa haombwi du´aa na wala haombwi uombezi; ni mamoja Mtume wala asiyekuwa yeye. Mambo yalivyo ni kwamba uombezi unaombwa kutoka kwake katika uhai wake kwa njia ya kwamba mtu anaweza kumwambia amwombee mbele ya Allaah, amwombee kwa Allaah kumponya mgonjwa wake, amrudishie kilichopotea na ampe hiki na kile. Vivyo hivyo siku ya Qiyaamah baada ya kukufuliwa na kukusanywa. Waumini watamwendea Aadam awaombee mbele ya Allaah ili Allaah ahukumu kati yao lakini ataombwa udhuru na atawaelekeza kwa Nuuh. Watamwendea Nuuh lakini na yeye ataomba udhuru. Kisha Nuuh atawaelekeza kwa Ibraahiym ambapo na yeye ataomba udhuru. Ibraahiym atawaelekeza kwa Muusa ambapo ataomba udhuru. Kisha Muusa atawaelekeza kwa ´Iysaa ambapo na yeye ataomba udhuru (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Halafu ´Iysaa atawaelekeza kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo wamwendee na aseme (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi ndiye mwenye nayo, mimi ndiye mwenye nayo.”

Atasogea mbele, atasujudu chini ya ´Arshi na amuhimidi Mola Wake sifa kubwa ambazo Allaah atamfungulia kisha atamwambia:

“Nyanyua kichwa chako, sema utasikizwa, ulizwa utapewa na ombea yatakubaliwa maombezi yako.”

Atawaombea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) watu waliosimamishwa kiwanjani ili wahukumiwe[12]. Vivyo hivyo atawaombea watu wa Peponi ili waingizwe Peponi. Kwa sababu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yupo. Lakini ndani ya kaburi baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haifai kumwomba uombezi, kumponya mgonjwa, kurudisha kilichopotea wala kitu kingine. Hali kadhalika wafu wengine hawaombwi kitu katika mambo haya. Bali wanaombewa du´aa na msamaha wakiwa ni waislamu. Mambo haya yanaombwa kutoka kwa Allaah (Subhaanah). Mfano muislamu anaweza kusema:

“Ee Allaah! Mwache Mtume Wako (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aniombee. Ee Allaah! Mponye mgonjwa wangu! Ee Allaah! Ninusuru dhidi ya adui yangu.”

na mfano wake. Kwa sababu Yeye (Subhaanah) amesema:

ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ

 “Niombeni Nitakuitikieni.”[13]

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ

“Watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi niko karibu Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba.”[14]

Kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kati yao.”[15]

Ni yenye kuenea kwa udhahiri wake. Haijuzu kwa waislamu kutoka nje ya Shari´ah ya Allaah. Bali ni lazima kwao kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah katika kila kitu katika yanayohusiana na ´ibaadah, mambo ya miamala na mambo mengine yote ya kidini na ya kidunia kwa sababu ni kuenea mambo yote hayo. Allaah (Subhaanah) amesema:

أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ ۚ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّـهِ حُكْمًا لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ

“Je, wanataka hukumu za kipindi cha kijahili? Na nani mbora zaidi kuliko Allaah katika kuhukumu kwa watu wenye yakini.”[16]

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri.”[17]

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio madhalimu.”[18]

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio mafasiki.”[19]

Aayah hizi ni zenye kuenea mambo yote ambayo watu wanakhitalafiana na kuzozana juu yake. Kwa ajili hii ndio maana akasema:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini… “

Bi maana watu katika waislamu na wengineo:

حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ

“… mpaka wakufanye wewe ni hakimu… “

Bi maana wewe Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivo inakuwa kwa kuhukumiana kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa uhai wake na kuhukumiana na Sunnah zake baada ya kufa kwake. Kuhukumiana na Sunnah yake ni kule kuhukumiana na yale yaliyoteremshwa ndani ya Qur-aan na Sunnah:

فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ

“… yale wanayozozana kati yao… “

Bi maana katika yale waliyozozana. Hili ndio la wajibu kwao wahukumiane kwa Qur-aan tukufu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kipindi cha uhai wake na baada ya kufa kwa kule kufuata Sunnah zake ambazo ndio zinaibainisha Qur-aan tukufu, kuitafsiri na kujulisha maana yake. Maneno Yake (Subhaanah):

ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“… kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kwa kujisalimisha.”[20]

Ni kwamba ni lazima ikunjuke mioyo yao juu ya hukumu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ndani ya vifua vyao kusibaki dukuduku juu ya hukumu aliyotoa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu hukumu yake ndio ya haki isiyokuwa na shaka yoyote na ndio hukumu ya Allaah (´Azza wa Jall).

Kwa hivyo ni lazima kujisalimisha kwake, mioyo ikunjukie jambo hilo na isihisi uzito wowote. Bali ni lazima kwao wajisalimishe juu ya jambo hilo kujisalimisha kikamilifu hali ya kuridhia na kuhisi utulivu hukumu ya Allaah. Haya ndio ya wajibu kwa waislamu wote katika yale wanayozozana katika madai na magomvi. Ni mamoja yanahusiana na mambo ya ´ibaadah, mali, ndoa, talaka au mengineyo. Imani hii iliyokanushwa ndio msingi wa imani ya kumwamini Allaah na Mtume Wake kwa nisba ya kuhukumiana na Shari´ah ya Allaah, kuridhika nayo na kuamini kuwa ndio hukumu stahiki kati ya watu. Kwa hivyo ni lazima yapatikane mambo haya.

Yeyote atakayedai kuwa inajuzu kuhukumu kwa kitu kingine, akaona kuwa inafaa kwa watu kuhukumiana na mababa, mababu na sheria za kibinadamu zilizotungwa na watu – pasi na kuja zimetoka wapi – anayedai kuwa kufanya hivo inafaa basi imani ni yenye kukanushwa kwake na anakuwa amekufuru ukafiri mkubwa. Mwenye kuona kuwa sio lazima kutumia Shari´ah ya Allaah wakati wa kuhukumu lakini bora ni ikiwa itatumiwa, akaona kuwa sheria zilizotungwa na watu ndio bora zaidi au akaona kuwa sheria zilizotungwa na watu zinalingana na hukumu ya Allaah anaritadi kutoka nje ya Uislamu.

Kwa hivyo kuna sampuli tatu:

1 – Shari´ah ndio bora. Lakini hapana vibaya kuhukumiana na isiyokuwa Shari´ah.

2 – Shari´ah na sheria zilizotungwa na watu zinalingana na hapana tofauti.

3 – Sheria zilizotungwa na watu ndio bora zaidi kuliko Shari´ah.

Aina hii ya tatu ndio mbaya zaidi. Zote ni ukafiri na kuritadi kutoka nje ya Uislamu.

Ama yule anayeona kuwa ni lazima kutumia Shari´ah ya Allaah wakati wa kuhukumu na kwamba haijuzu kuhukumu kwa kanuni na mambo mengine yanayokwenda kinyume na Shari´ah ya Allaah, lakini pengine akahukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah kutokana na matamanio ndani ya nafsi yake dhidi ya yule muhukumiwa, rushwa, mambo ya kisiasa au sababu nyengine miongoni mwa sababu na wakati huohuo anatambua kuwa yeye ni dhalimu, mwenye kukosea na mwenye kwenda kinyume na Shari´ah, basi huyu imani yake inakuwa pungufu na imekanushwa kwake kule kukamilika kwa imani ya wajibu. Anakuwa kafiri ambaye amekufuru kufuru ndogo, dhalimu ambaye amedhulumu dhuluma ndogo, fasiki ambaye amefanya ufuska mdogo, kama ilivyosihi maana ya hayo kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa), Mujaahid na kikosi kutoka kwa Salaf (Rahimahumu Allaah). Aidha ndio mtazamo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah tofauti na wanavoona Khawaarij, Mu´tazilah na wale waliofuata njia yao.

[1] 04:64-65

[2] 04:64

[3] 81:29

[4] 02:21

[5] 04:26

[6] 04:64

[7] 04:64

[8] al-Bukhaariy (1864) na Muslim (1397).

[9] Muslim (1631).

[10] Ahmad (15729), Abu Daawuud (1047), an-Nasaa´iy (1374) na Ibn Maajah (1085).

[11] Ahmad (4198) na an-Nasaa´iy (1282).

[12] al-Bukhaariy (7510) na Muslim (193).

[13] 40:60

[14] 02:186

[15] 04:65

[16] 05:50

[17] 05:55

[18] 05:45

[19] 05:47

[20] 04:65

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 62-70
  • Imechapishwa: 07/07/2022