Upokezi wa Muusa bin ´Uqbah kutoka kwa Ishaaq bin Yahyaa, kutoka kwa ´Ubaadah bin as-Swaamit kuna ziada nzuri. Moja wapo ni ile aliyotusimulia Abu Ya´laa Hamzah bin ´Abdil-´Aziyz al-Muhallabiy: ´Abdullaah bin Muhammad ar-Raaziy ametuhadithia: Abu ´Uthmaan Muhammad bin ´Uthmaan bin Abiy Suwayd ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan (bin al-Mubaarak) ametuhadithia: Fudhwayl bin Sulaymaan ametuhadithia, kutoka kwa Muusa bin ´Uqbah, kutoka kwa Ishaaq bin Yahyaa, kutoka kwa ´Ubaadah bin as-Swaamit, aliyeeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) hushuka kila usiku katika mbingu ya chini wakati kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku na kusema: ”Kuna mja miongoni mwa waja Wangu anayeniomba Nikamuitikia? Je, kuna ambaye ameidhulumu nafsi yake Nikamsamehe? Je, kuna ambaye riziki yake imekuwa ya dhiki akaniomba Nikamruzuku? Je, kuna dhalimu atanitaja ambapo Nikamnusuru? Je, kuna ambaye ni dhalimu wa nafsi yake akaniomba nikamwacha huru?” Anafanya hivo mpaka kupambazuke asubuhi, ambapo Akapanda juu ya Kursiy Yake.”[1]

Vivyo hivyo katika upokezi wa Abuz-Zubayr kutoka kwa Jaabir, kupitia kwa Marzuuq Abu Bakr, ambao umepokelewa na Muhammad bin Ishaaq bin Khuzaymah kwa ufupi.

Vivyo hivyo katika upokezi wa Ayyuub kutoka kwa Abuz-Zubayr, kutoka kwa Jaabir, ambao umepokelewa na al-Hasan bin Sufyaan katika ”al-Musnad” yake.

Vivyo hivyo katika upokezi wa Hishaam ad-Dastawaa-iy kutoka kwa Abuz-Zubayr, kutoka kwa Jaabir, aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mpaka jioni ya ´Arafah Allaah hushuka katika mbingu ya chini, akajifakharisha kwa ajili ya watu wa ardhini mbele ya wakazi wa mbinguni na kusema: ”Watazameni waja Wangu; wamekuja hali ya kuwa timtim na vumbi juani. Wamekuja kutokea kila kona ya mbali. Wanataraji rehema Zangu na bado hawajaona adhabu Yangu.” Hakuna siku ambayo Allaah amewaacha watu huru na Moto zaidi kama siku ya ´Arafah.”

[1] al-Haythaymiy amesema:

“at-Twabaraaniy amepokea mfano wake katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” na “al-Mu´jam al-Awsatw”. Yahyaa bin Ishaaq hakusikia chochote kutoka kwa ´Ubaadah na Muusa bin ´Uqbah pekee ndiye kasimulia kutoka kwake. Wasimulizi wengine wote katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” ni wasimulizi wa Swahiyh.” (Majma´-uz-Zawaa’id (10/154))

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 212-214
  • Imechapishwa: 06/12/2023