15. Fitina juu ya kuumbwa kwa Qur-aan

Kwa kifupi ni kwamba Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanasema kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na hayakuumbwa. Walipewa mtihani mkubwa wakati wa al-Ma´muun, al-Mu´taswim na al-Waathiq kwa sababu ya hilo. Hawa walikuwa ni makhalifa wa ´Abbaasiyyah. Walipewa mtihani mkubwa kama tulivyosema. Jahmiyyah na Mu´tazilah waliishika nchi na wakawa na vyeo katika zama za al-Ma´muun, al-Mu´taswim na al-Waathiq. Wao ndio walikuwa na neno. Wakawa na uongozi juu ya Ahl-us-Sunnah na wakawataka wasema kuwa Qur-aan imeumbwa. Waliwalazimisha hilo. Yule asiyesema hivo anafukuzwa kazini kwake. Aliyekuwa ametoka kwenye Jihaad katika njia ya Allaah na akashikwa mateka alikuwa haachwi mpaka aseme kuwa Qur-aan imeumbwa. Asiyefanya hivo anaendelea kufanywa mateka kwa makafiri. Baadhi walitekswa, wengine wakauawa, wengine wakatiwa jela na kadhalika.

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) alimuwafikisha na kumfanya imara Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah). Kamwe hakusema batili. Hakutikiswa kutokamana na neno la haki. Pindi walipokuwa wakitaka kujadiliana nae alikuwa akiwaambia:

“Nileteeni dalili kutoka katika Kitabu cha Allaah au Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Hawawezi kuleta dalili yoyote kutoka katika Kitabu cha Allaah wala kutoka katika Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba Qur-aan imeumbwa. Akijadiliana nao na akawaraddi kwa hoja na dalili kutoka katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

´Abdul-´Aziyz al-Kinaaniy, mwandishi wa kitabu “al-Haydah”, alijadiliana nao na akawaponda. ´Abdullaah bin Muhammad al-Hadhwramiy alijadiliana nao na akawaponda.

Wakati wa zama za al-Mutawakkil, ambaye naye alikuwa ni khalifa wa ´Abbaasiyyah, ndipo fitina hii ikazimika. Allaah amjaze na kumlipa kheri nyingi. Alizima fitina hii ya Jahmiyyah na Mu´tazilah na akainusuru haki. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) akawatia nguvu Ahl-us-Sunnah kwa kumfanya akaweza kuwaponda watu wa batili. Allaah amrehemu.

Ash´ariyyah na Kullaabiyyah wanasema kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah, lakini ni Qur-aan ipi? Wanasema ni maana ya ndani iliyosimama kwenye dhati ya Allaah na haina herufi na sauti. Haya ni maneno batili yanayoraddiwa na Qur-aan na Sunnah. Kama tulivyosmea Allaah anazungumza na hakuacha daima kuwa ni mwenye kuzungumza. Kuna dalili nyingi juu ya hilo. Katika maneno Yake ni pamoja na Qur-aan iliyoteremshwa kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ

“Haitokifikia ubatili mbele yake na wala nyuma yake! [Hapana,] ni uteremsho kutoka kwa Mwenye hikmah wa yote, Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote.” 41:42

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 15/10/2016