16. Qadar ni yenye kutoka kwa Allaah

Abu Muhammad ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Haatim amesema:

3- Qadar, kheri na shari yake, ni yenye kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall).

MAELEZO

Qadar, kheri na shari yake, ni yenye kutoka kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Hakukuwi katika ufalme wa Wake isipokuwa kile anachokitaka. Hakuna mwingine anayeumba viumbe hawa isipokuwa Allaah. Hakukuwi katika ulimwengu huu harakati wala utulivu isipokuwa Allaah ndiye kauumba. Hakuna chochote katika hayo kinachokuwa ispokuwa kwa kutaka na kupenda Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Ujuzi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni wa milele. Aliyajua ni yepi viumbe Wake watafanya. Amekadiria riziki zao, muda wao wa kuishi na matendo yao. Alijua siku zote yatayopitika. Aliyajua hayo na kisha baada ya hapo akayaandika kwenye Ubao uliohifadhiwa:

إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ ۚ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ

“Hakika Sisi tunahuisha maiti na tunaandika yale waliyoyatanguliza na athari zao; kila kitu Tumekirekodi barabara katika daftari linalobainisha.” 36:12

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” 57:22

Kitabu kinachokusudiwa hapa ni Ubao uliohifadhiwa. Viumbe na misiba yote imeandikwa kwenye kitabu hicho kabla ya havijaumbwa. Allaah ameshayakadiria:

وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ

“Kila kitu Tumekirekodi barabara katika daftari .” 36:12

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

“Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa makadirio.” 54:49

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) aliyajua matendo ya viumbe, akaumba matendo yao na akayakadiria. Daima alijua yaliyokuwepo na yatayokuwepo. Hakuna harakati wala utulivu wowote wenye kutoka kwa Malaika, majini, watu na wanyama isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) aliyajua na akayaumba. Hakuna chochote chenye kufichika Kwake. Hakuna kinachompita. Yote hayo yameandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 15/10/2016