Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya uombezi ni maneno Yake (Ta´ala):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Na wanaabudu asiyekuwa Allaah ambao [hawawezi] kuwadhuru na wala kuwanufaisha na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[1]

Kuna aina mbili za uombezi:

1 – Uombezi wenye kukanushwa.

2 – Uombezi wenye kuthibitishwa.

Uombezi wenye kukanushwa ni ule wenye kutafutwa kutoka kwa asiyekuwa Allaah katika yale yasiyoweza kufanya yeyote isipokuwa Allaah. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ ۗ وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Enyi mlioamini! Toeni sehemu katika vile Tulivyokuruzukuni kabla haijafika siku ambayo hakutakuweko mapatano [ya fidiya] humo wala urafiki wala uombezi na makafiri wao ndio madhalimu.”[2]

Uombezi wenye kuthibitishwa ni ule wenye kutafutwa kutoka kwa Allaah na mwombezi amekirimiwa uombezi na muombewaji ni yule ambaye Allaah ameridhia maneno yake na vitendo vyake baada ya kupewa idhini. Amesema (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?”[3]

MAELEZO

Kuna aina mbili za uombezi; uombezi wenye kukanushwa na uombezi wenye kuthibitishwa:

1 – Uombezi wenye kuthibitishwa ni ule ambao unaombwa kutoka kwa asiyekuwa Allaah katika mambo ambayo hakuna ayawezaye isipokuwa Allaah. Ni uombezi batili, wenye kupingwa na hauwezi kutokea. Hakuna mwenye uwezo nao isipokuwa Allaah pekee. Waungu hawa hawawezi kuombea mbele ya Allaah. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?”[4]

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“Na wala hawamuombei uombezi yeyote yule isipokuwa yule Anayemridhia.”[5]

Mfano wa uombezi wenye kukanushwa na wa batili ni kuomba uombezi kutoka kwa masanamu, mawe au mtu akamuomba ´Aliy, al-Badawiy na al-Husayn wawafanyie uombezi.

[1] 10:18

[2] 02:254

[3] 02:255

[4] 02:255

[5] 21:28

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 138
  • Imechapishwa: 06/03/2023