Umebarikika na Umetukuka Mola wetu – Huku ni kumsifu Allaah kwa mambo mawili:

1 – Tabarruk. Herufi (التاء) ni kwa njia ya kupindukia. Allaah (´Azza wa Jall) ndiye anayestahiki baraka.

2 – Umebarikika – Maana yake ni kwamba zimekuwa nyingi kheri Zako na zimewaenea viumbe. Kwa sababu tumekwishatangulia kusema kuwa baraka ni kheri nyingi na zenye kudumu.

”Mola wetu.”

Kwa maana ya kwamba ´Ee Mola wetu`. Ni wito ambao umeondoshewa ´ee` ya kuita.

”Umetukuka Mola wetu.”

Ujuu wa kidhati na wa kisifa. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko juu kwa dhati na kwa sifa Zake. Yuko juu ya viumbe wote kwa dhati Yake. Aidha ujuu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) ni sifa ya kidhati, kimilele na ya siku zote. Lakini kulingana Kwake juu ya ´Arshi ni sifa ya kimatendo inayohusiana na matakwa Yake (Subhaanahu wa Ta´ala). ´Arshi ndio kiumbe kilicho juu zaidi na Allaah amelingana juu yake. Kwa maana ya kwamba Yuko juu yake ujuu unaolingana na utukufu na ukuu Wake. Hatupekui namna ya sifa hiyo na wala hatuipigii mifano. Salaf wameafikiana kuhusu ujuu huo kwa sababu Qur-aan, Sunnah, akili na maumbile yamejulisha hivo[1]. Kuhusu ujuu wa kisifa maana yake ni kwamba Allaah anazo sifa kamili zilizo kuu na kamilifu zaidi na kwamba haiyumkiniki kukawepo upungufu wowote katika sifa Zake kwa njia yoyote ile.

[1] Rejea utafiti huo katika maelezo ya ”al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah” ya Shaykh wetu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Du´aa´ al-Qunuut-il-Witr, uk. 18-20
  • Imechapishwa: 22/03/2024