14. Ni ipi Hijaab inayokubalika kwa mujibu wa Shari´ah?

Swali 14: Ni ipi Hijaab inayokubalika kwa mujibu wa Shari´ah?

Jibu: Hijaab inayokubalika kwa mujibu wa Shari´ah ni mwanamke kufunika yale anayoharamika kuyaonyesha. Kinachoshika nafasi ya kwanza ni kufunika uso, kwa sababu ndio sababu inayopelekea katika fitina na matamanio. Kwa hivyo ni lazima kwa mwanamke kuufunika uso wake mbele ya wasiokuwa Mahram zake. Kuhusu wale waliodai kuwa Hijaab inayokubalika kwa mujibu wa Shari´ah ni kufunika tu shingo, mgongo, miguu, miundi na mikono na akamruhusu mwanamke kuonyesha uso na viganja vyake vya mikono, ni miongoni mwa maoni yanayostaajabisha mno. Ni jambo linalotambulika kuwa matamanio na mahali palipo na fitina ni usoni. Ni vipi mtu anaweza kusema kuwa Shari´ah inamkataza mwanamke kuonyesha miguu halafu imruhusu kuonyesha uso? Hili ni jambo lisilowezekana katika Shari´ah tukufu na yenye hekima iliyotakasika kutokamana na mgongano.

Kila mtu anatambua kuwa fitina inayopatikana kwa kuonyesha uso ni kubwa zaidi kuliko fitina inayopatikana kwa kunyesha miguu. Kila mtu anajua kuwa matamamio ya wanamme juu ya wanawake yako usoni. Kwa ajili hiyo endapo ataambiwa yule mposaji kuwa mwanamke anayetaka kumposa sura yake ni mbaya, lakini hata hivyo miguu yake ni mizuri, basi hatomposa. Na endapo ataambiwa kuwa sura yake ni nzuri, lakini pamoja na hivyo mikono yake, viganja vyake vya mikono, miguu yake, miundi yake si mizuri sana, atamposa. Kwa ajili hiyo inapata kufahamika kuwa uso ndio kitu cha kwanza kinachotakiwa kufunikwa. Aidha zipo dalili ndani ya Kitabu cha Allaah, Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), maneno ya Maswahabah pamoja maneno ya maimamu na wanazuoni wa Uislamu zinazojulisha ulazima wa mwanamke kuufunika mwili wake mzima mbele ya wale wasiokuwa Mahram zake. Vilevile dalili hizo zinafahamisha kuwa ni lazima kwa mwanamke kuufunika uso wake mbele ya wasiokuwa Mahram zake, jambo ambalo hapa si mahali pake pa kulitaja na Allaah ndiye anajua zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 23
  • Imechapishwa: 01/03/2023