13. Ni ipi hukumu ya kusikiliza muziki na nyimbo pamoja na vipindi vya TV ambapo wanawake wanaonyesha mapambo yao?

Swali 13: Ni ipi hukumu ya kusikiliza muziki na nyimbo pamoja na vipindi vya TV ambapo wanawake wanaonyesha mapambo yao?

Jibu: Kusikiliza muziki na nyimbo ni haramu na hapana shaka juu ya uharamu wake. Imepokelewa kutoka kwa Salaf, ambao ni Maswahabah na wanafunzi wao, ya kwamba muziki unazalisha unafiki ndani ya moyo, maneno ya kipuuzi na unapelekea mtu kuegemea juu yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ

“Miongoni mwa watu wako ambao hununua maneno ya upuuzi ili wapoteze kutokamana na njia ya Allaah pasi na elimu na huichukulia mzaha – hao watapata adhabu ya kutweza.”[1]

Ibn Mas´uud amesema wakati alipokuwa anafasiri Aayah hii:

“Naapa kwa Allaah ambaye hakuna mungu wa haki mwingine isipokuwa Yeye; ya kwamba ni nyimbo.”[2]

Tafsiri ya Swahabah ni hoja na iko katika ngazi ya tatu katika tafsiri, kwa sababu tafsiri ina ngazi tatu:

1 – Tafsiri ya Qur-aan kwa Qur-aaan.

2 –  Tafsiri ya Qur-aan kwa Sunnah.

3 – Tafsiri ya Qur-aan kwa maneno ya Maswahabah.

Wapo mpaka baadhi ya wanazuoni wenye kuona kuwa tafsiri ya Swahabah ina hukumu moja kama ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini maoni ya sawa ni kwamba haina hukumu moja. Lakini hata hivyo ndio maneno yaliyo karibu zaidi na haki.

Isitoshe ni kwamba kusikiliza nyimbo na muziki ni kutumbukia katika yale ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha pale aliposema:

“Hakika watakuweko katika Ummah wangu watu wataohalalisha uzinzi, hariri, pombe na zana za muziki.”

Bi maana wataona kuwa uzinzi, pombe na hariri ni halali. Ni wanaume ambao haifai kwao kuvaa hariri. Zana za muziki ni ala za upuuzi. Ameipokea al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Maalik al-Ash´ariy au Abu ´Amr al-Ash´ariy. Kutokana na hilo mimi nawatahadharisha ndugu zangu waislamu kusikiliza nyimbo na muziki na wala wasidanganyike na maoni ya baadhi ya wanazuoni waliosema kuwa zana za muziki zinafaa. Kwa sababu dalili zinazoharamisha ziko wazi kabisa.

Kuhusu kuangalia vipindi vya TV ambavyo wanaonekana wanawake ni haramu muda wa kuwa zinapelekea katika fitina na kuwa na mafungamano na wanawake. Mara nyingi vipindi vyote vya TV ni vyenye madhara hata kama mwanamme hamuoni mwanamke na mwanamke hamuoni mwanaume. Kwa sababu malengo yake huwa ni kuidhuru jamii katika maadili na tabia yake. Namuomba Allaah (Ta´ala) awakinge waislamu kutokana na shari yake na awatengeneze watawala wa waislamu katika yale yanayozitengeneza hali za waislamu na Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] 31:06

[2] al-Bukhaariy na wengineo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 01/03/2023