14. Mifano ya hekima katika kulingania II

3 – Mfano wa tatu: Kuna bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimeangamia!” Akasema: “Kipi kimekuangamiza? Akajibu: “Nimemwingilia mke wangu ndani ya Ramadhaan na mimi nimefunga.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwamrisha aache mtumwa huru.” Akasema: “Simpati.” Kisha akamwamrisha afunge miezi miwili mfululizo. Akasema: “Siwezi.” Kisha akamwamisha afunge miezi miwili mfululizo. Akasema: “Siwezi.” Bwana yule akaketi chini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja na tende na kumwambia: “Zichukue ukatoe swadaqah.” Bwana yule akawa na matumaini ya ukarimu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ndiye kiumbe mkarimu zaidi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mkarimu zaidi ya watu. Bwana yule akasema: “Hivi kuna ambaye ni fakiri zaidi kuliko mimi, ee Mtume wa Allaah? Ninaapa kwa Allaah hakuna kati ya milima miwili hii watu wa nyumba ambao ni mafukara zaidi kuliko mimi.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka yakaonekana magego yake.”

Kwa sababu mtu huyu amekuja hali ya kuwa ni mwenye kuogopa na kusema: “Nimeangamia.” Akaondoka hali ya kuwa amevuna. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Walishe watu wa nyumbani kwako.”[1]

Bwana yule akaondoka hali ya kuwa ni mwenye utulivu, mwenye kuvuna na mwenye kufurahi na dini hii ya Kiislamu na kwa wepesi huu wa mlinganizi huyu juu ya dini hii ya Kiislamu – swalah na amani ziwe juu yake.

4 – Mfano wa nne: Hebu wacha tuangalie ni namna gani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitangamana na mwenye kutenda dhambi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona bwana mmoja ambaye mkononi mwake kulikuwa na pete ya dhahabu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaitoa kwa mkono wake mtukufu na akaitupa ardhini na akasema:

“Hivi kweli mmoja wenu anakusudia kaa la moto na kuliweka mkononi mwake?”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakutangamana naye kama wale wa mwanzo. Bali aliiondosha kutoka mkononi mwake na akaitupa ardhini. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipogeuka na kuondoka zake bwana yule akaambiwa achukue pete yake na anufaike nayo. Akasema:

“Naapa kwa Allaah! Sichukui pete aliyoitupa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

 Allaah ni mkubwa! Huku ni kujisalimisha kukubwa walikokuwa nako Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

Muhimu ni kwamba ni lazima kwa mlinganizi alinganie kwa Allaah kwa hekima. Mjinga si kama mwanazuoni. Mkaidi sio kama yule mwenye kujisalimisha. Kila mahali kuna maneno yake na kila nafasi ina hali yake.

[1] al-Bukhaariy (1936) na Muslim (1111).

[2] Muslim (2090).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 20
  • Imechapishwa: 04/11/2021