13. Mifano ya hekima katika kulingania

Hekima inakataa ulimwengu kubadilika papo hapo. Ni lazima jambo lichukue muda mrefu. Mkabili ndugu yako ambaye wewe hii leo unamlingania katika haki. Nenda naye kidogo kidogo mpaka umwondoe kutoka katika batili. Watu kwako wasiwe katika kiwango kimoja. Kuna tofauti kati ya mjinga na mkaidi.

Pengine ni jambo munasibu kupiga mfano wa ulinganizi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

 1 – Mfano wa kwanza. Aliingia mbedui mmoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameketi msikitini na Maswahabah zake. Mbedui yule akakojoa kandoni na msikitini ambapo watu wakamkemea na kumkaripia kwa ukali. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), naye ndiye ambaye Allaah amempa hekima, akawakataza. Alipomaliza kukojoa akaamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwagia juu yake ndoo ya maji. Madhara yakaondoka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwita yule mbedui na kumwambia:

“Hakika misikiti hii hakusilihi ndani yake kitu katika dhara au uchafu. Hakika si venginevyo imetengwa kwa ajili ya swalah na usomaji Qur-aan.”[1]

Au (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema maneno yanayofanana na hayo. Kikakunjuka kifua cha yule mbedui kwa matangamano haya mazuri. Kwa ajili hiyo nimewaona baadhi ya wanazuoni wakisema kwamba mbedui huyo alisema:

“Ee Allaah! Nirehemu mimi na Muhammad na usirehemu pamoja nasi mwengine yeyote.”

Kwa sababu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitangamana naye matangamano haya mazuri. Ama Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walijaribu kuondosha uovu pasi na kukisia hali ya bwana huyu mjinga.

2 – Mfano wa pili: Mu´aawiyah bin al-Hakam (Radhiya Allaahu ´anh) alikuja wakati ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anawaswalisha watu. Akachemua bwana mmoja na kumhimidi Allaah. Anapokwenda chafya mtu ndani ya swalah basi amuhimidi Allaah. Ni mamoja amesimama, yuko katika Rukuu´ au katika Sujuud. Bwana huyo akamuhimidi Allaah. Mu´aawiyah akasema:

يرحمك الله

“Allaah akurehemu.”

Huku ni kumzungumzisha mwanadamu, jambo ambalo linaharibu swalah. Watu wakamtupia macho na wakawa ni wenye kumtazama. Mu´aawiyah akasema:

“Akukose mama yako.”

Maneno haya yanasemwa lakini hata hivyo hakukusidiwi maana yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyasema kumwambia Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) wakati aliposema: “Je, nisikujuze kitu kinachomiliki yote hayo?” Akasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah.” Akamwambia: “Jizuilie na huu.” ambapo akaushika ulimi wake. Mu´aadh akasema: “Kwani tutachukuliwa hatua kwa yale tunayoyatamka?” Akasema:

“Akukose mama yako, ee Mu´aadh. Je, watu watavugumizwa Motoni juu ya nyuso zao” au alisema “juu ya pua zao kama sio kwa sababu ya mavuno ya ndimi zao?”[2]

Mu´aawiyah (Radhiya Allaahu ´anh) akaendelea na swalah yake. Alipomaliza kuswali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwita. Mu´aawiyah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Naapa kwa Allaah sijapatapo kuona mwalimu anayefunza vizuri kama yeye. Swalah na amani ziwe juu yake. Naapa kwa Allaah hakunikaripia wala kunishambulia. Alichosema ni:

“Hakika swalah hii hakusilihi ndani yake chochote katika maneno ya watu. Hakika si venginevyo ndani yake kuna Tasbiyh, Takbiyr na kusoma Qur-aan.”[3]

Au (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema maneno yanayofanana na hayo. Tazama ulinganizi wenye kupendwa na nafsi anayoikubali mtu na kifua chake kinakuwa kikunjufu.

Tunachukua kutoka katika Hadiyth faida ya ki-Fiqh; ambaye atazungumza ndani ya swalah pasi na kujua ni kwamba maneno yanabatilisha swalah. Lakini yeye swalah yake ni sahihi.

[1] al-Bukhaariy (219), (221), (625) na Muslim (285).

[2] Ahmad (22366), at-Tirmidhiy (2616) na Ibn Maajah (3973).

[3] Muslim (537).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 04/11/2021