14. Kutaka uokozi kwa asiyekuwa Allaah au kumuomba mwingine asiyekuwa Yeye ni katika shirki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ

“Wala usiombe badala ya Allaah asiyekufaa na wala asiyekudhur; na ukifanya hivyo, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu. Allaah akikugusisha dhara, basi hakuna awezaye kuiondosha isipokuwa Yeye.” (Yuunus 10:106-107)

2-

فَابْتَغُوا عِندَ اللَّهِ الرِّزْقَ وَاعْبُدُوهُ وَاشْكُرُوا لَهُ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

”Basi tafuteni riziki kwa Allaah na mwabuduni na mshukuruni; Kwake ndio mtarejea.” (al-´Ankabuut 29:17)

3-

وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّن يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَن لَّا يَسْتَجِيبُ لَهُ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَهُمْ عَن دُعَائِهِمْ غَافِلُونَ

“Ni nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayemwomba badala ya Allaah, ambao hatowaitikia mpaka siku ya Qiyaamah nao hawatambui maombi yao.” (al-Ahqaaf 46:05-06)

4-

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ

”Au Yule anayemuitika mwenye dhiki anapomwomba na akamuondoshea uovu?” (an-Naml 27:62)

5- at-Twabaraaniy amepokea kwa cheni ya wapokezi wake:

“Katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kulikuwepo mnafiki akiwaudhi waumini. Baadhi yao wakasema: “Simameni tumwendee Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumtaka msaada kutokana na mnafiki huyu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hakika mimi siye niombwaye uokozi. Isipokuwa uokozi unaombwa kwa Allaah pekee.”[1]

MAELEZO

Mlango huu ni maalum baada ya ujumla uliotangulia. Kwa sababu kutaka uokozi ni katikad du´aa. Kila mwenye kuomba uokozi anakuwa ameomba na si kila mwenye kuomba anakuwa ameomba uokozi. Mtu anayeomba uokozi ni yule anayeomba wakati wa matatizo, kama ilivyotajwa katika Aayah:

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ

“Akamsaidia yule ambaye katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake.” (al-Qaswasw 28:15)

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ

“Pindi mlipomuomba uokovu Mola wenu.” (al-Anfaal 08:09)

Yule ambaye ni mgonjwa au anaogopa kuzama ndani ya maji na akaomba uokozi kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kwa al-Badawiy amefanya shirki kubwa. Washirikina wakati wa kipindi cha kikafiri walikuwa wakimuomba Allaah peke yake wakati wa matatizo. Kwa sababu walikuwa wakijua kuwa hakuna awezaye kuwaokoa isipokuwa Allaah pekee. Kuhusu washirikina katika wakati wetu huu wanashirikisha katika kipindi cha raha na katika kipindi cha matatizo. Yule anayefanya hivo wakati wa matatizo anazingatiwa ametaka uokozi  na yule anayefanya hivo wakati wa raha anazingatiwa ameomba. Lakini hivyo matendo yote mawili ni shirki. Dalili ya hayo ni:

1-

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ

“Wala usiombe badala ya Allaah asiyekufaa na wala asiyekudhur; na ukifanya hivyo, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.”

Bi maana miongoni mwa washirikina.

 وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Makafiri wao ndio madhalimu.” (al-Baqarah 02:254)

Allaah amebainisha hukumu juu ya yule mwenye kuomba badala ya Allaah kisichoweza kumnufaisha wala kumdhuru. Hukumu hii ni yenye kuenea na inawahusu viumbe wote wasioweza kunufaisha wala kudhuru wao wenyewe. Allaah ndiye awezaye kudhuru na kunufaisha kivyake. Allaah amebainisha kwamba yule mwenye kumuomba asiyekuwa Allaah basi ni mshirikina. Hata hivyo kunavuliwa katika hayo yule mwenye kumuomba aliyehai, muweza na wakati huohuo yuko mbele yake. Waislamu wameafikiana kwamba sio shirki. Mfano wa hilo ni kama mtu akamuomba mwingine kubeba kitu, kumsaidia kutua kitu chini na mfano wa hayo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ

“Allaah akikugusisha dhara, basi hakuna awezaye kuiondosha isipokuwa Yeye.”

Haya ni kujengea juu ya kwamba viumbe si waweza wa kuleta manufaa wala kuzuia madhara. Vipi mtu atamuabudu mwingine asiyekuwa Yeye ilihali si muweza?

2-

فَابْتَغُوا عِندَ اللَّهِ الرِّزْقَ وَاعْبُدُوهُ وَاشْكُرُوا لَهُ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

”Basi tafuteni riziki kwa Allaah na mwabuduni na mshukuruni; Kwake ndio mtarejea.”

Ameamrisha riziki na uokozi aombwe Yeye peke yake na asiabudiwe mwingine yeyote asiyekuwa Yeye. Kunavuliwa katika hayo yale yaliyotangulia.

3-

وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّن يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَن لَّا يَسْتَجِيبُ لَهُ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَهُمْ عَن دُعَائِهِمْ غَافِلُونَ

“Ni nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayemwomba badala ya Allaah, ambao hatowaitikia mpaka siku ya Qiyaamah nao hawatambui maombi yao.”

Aayah inathibitisha kwamba hakuna yeyote ambaye ni mpotevu zaidi kuliko yule anayemwomba mwingine asiyekuwa Allaah. Mtu kama huyo hakufaulu hapa duniani na huko Aakhirah ni mwenye kukhasirika na kutupwa Motoni. Ameeleza mambo mane kuhusu yule mwenye kumuomba badala ya Allaah:

1- Hawawezi kumuitikia mpaka siku ya Qiyaamah.

2- Hawatambui maombi yao. Imaa kwa sababu ni wafu, vitu visivyokuwa na uhai na havina hisia, wako hai lakini wameshughulishwa au Malaika wasiotambua ni nani mwenye kuwaomba.

3- Watakuwa ni maadui wa wale wawaombao siku ya Qiyaamah.

4- Watajitenga mbali na ´ibaadah zao na kuzikemea.

 أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ

”Au Yule anayemuitika mwenye dhiki anapomwomba na akamuondoshea uovu?”

Bi maana hakuna yeyote awezaye hayo. Kwa ajili hiyo haitakikani kumuomba yeyote asiyekuwa Allaah.

 5- at-Twabaraaniy amepokea kwa cheni ya wapokezi wake:

“Katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kulikuwepo mnafiki akiwaudhi waumini. Baadhi yao wakasema: “Simameni tumwendee Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumtaka msaada kutokana na mnafiki huyu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hakika mimi siye niombwaye uokozi. Isipokuwa uokozi unaombwa kwa Allaah pekee.”

Imekuja katika upokezi mwingine kwamba ´Ubaadah bin as-Swaamit ndiye aliyesema hivo na kwamba mnafiki huyo alikuwa ´Abdullaah bin Abiy Saluu. Hata hivyo katika cheni ya wapokezi wake kuna baadhi ya udhaifu.

Maswahabah hawakumuomba uokozi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa ni kwa sababu walijua kuwa anaweza kuwaokoa naye aidha kwa kumuua au kumfunga. Walitambua kuwa inafaa kumuomba msaada ambaye yuhai na muweza. Kwa ajili hiyo ndio maana wakaenda kwake. Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Hakika mimi siye niombwaye uokozi” yanaweza kufasiriwa kwa njia mbili:

1- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawezi kumuua kwa sababu ilikuwa imekatazwa ili watu wasije kusema kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anawaua Maswahabah wake. Kwa ajili hiyo ndio maana akaacha kumuua.

2- Upokezi huu ukiwa ni Swahiyh basi inawezekana alisema hivo kwa sababu ya kuziba njia ijapokuwa alikuwa ni muweza wa kuwaondoshea naye. Alisema hivo ili wasitamke namna hiyo katika mambo asiyoyaweza.

Kinacholengwa ni kwamba uokozi hauombwi kutoka kwa mwingine asiyekuwa Allaah isipokuwa katika yale mambo ambayo aliyehai anayaweza.

[1] al-Haytamiy amesema: ”Ameipokea at-Twabaraaniy. Wanaume wake ni wanaume wa al-Bukhaariy isipokuwa Ibn Lahiy´ah ambaye hata hivyo hupokea Hadiyth nzuri.” (Majma´-uz-Zawaa-id (17276)).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 54-56
  • Imechapishwa: 02/10/2018