14. Kujisalimisha juu ya yale yote yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mfano wa Hadiyth hizo ni Hadiyth ya “mkweli na msadikishwaji” na Hadiyth kuhusu Qadar na Hadiyth nyengine zote kuhusu Kuonekana. Haijalishi kitu hata kama kuna ambao hawawezi kuzisikia au kuchukulia kwa ubaya kuzisikiza.”

MAELEZO

Hadiyth ya mkweli na msadikishwaji ni ile Hadiyt ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) isemayo:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ni mkweli na mwenye kusadikishwa, ametueleza: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu. Kisha huwa donge la damu kwa muda kama huo. Kisha huwa pande la nyama kwa muda kama huo. Kisha Allaah humtumia Malaika na akampulizia roho na akaamrishwa aandike maneno manne; riziki yake, muda wake wa kuishi, matendo yake na kama atakuwa mtu muovu au mwema.”[1]

Qadar imeandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa. Kama ilivyokuja katika ile Hadiyth iliotangulia:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika!” Kuanzia hapo ikaandika yote yatayokuwepo mpaka kisimame Qiyaamah.”[2]

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

”Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa Qadar.”[3]

Allaah ameandika kwenye Ubao uliohifadhiwa makadirio ya kila kitu, mpaka kushindwa na werevu, kabla ya kuumba mbingu na ardhi. Kwa hiyo ni wajibu kwetu kuyaamini hayo.

Imepokelewa kwamba Malaika watukufu wanakuwa pamoja na waja na huandika kila kitu kinachotoka kwao. Halafu wanarudi juu mbinguni na wanatazama kwenye Ubao uliohifadhiwa na kuona kwamba yale yote waliyoandika yanaenda sambamba na yale yaliyomo kwenye Ubao uliohifadhiwa. Kila siku ya jumatatu na alkhamisi maandishi haya huonyeshwa Allaah (´Azza wa Jall)[4] ambapo Allaah hufuta yale yote yasiyopelekea katika thawabu wala adhabu kama mfano wa “Teremsha soga, nipe mapenzi na nipe maji”. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَمْحُو اللَّـهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِندَهُ أُمُّ الْكِتَابِ

“Allaah anafuta yale ayatakayo na anathibitisha na Kwake ndiko kuna Mama wa Kitabu.”[5]

Haya ni yale makadirio ya milele. Kuna makadirio vilevile ya umri na ni yale yaliyotajwa katika Hadiyth ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh). Baada ya hapo kunakuja makadirio ya mwaka yanayoandikwa katika usiku wa Qadar. Hapo ndipo Malaika wanaandika yale yote yatayowapitikia waja katika mwaka. Makadirio haya yanazingatiwa ni utekelezaji wa makadirio ya milele. Halafu kunakuja makadirio ya siku na hayo ni yale yanayotoka kwa waja katika siku yao hiyo. Hayo pia huandikwa na Malaika. Makadirio hayo pia yanazingatiwa ni utekelezaji wa makadirio ya milele.

[1] al-Bukhaariy (6549) na Muslim (2643).

[2] Abu Daawuud (4700) na at-Tirmidhiy (2155). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (2017).

[3] 54:49

[4] at-Tirmidhiy (747). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (1041).

[5] 13:39

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 96-97
  • Imechapishwa: 09/04/2019