14. Kifunguzi cha tatu cha swawm: Sindano za lishe na kutiwa damu

3 – Vile vitu vilivyo na maana ya kula na kunywa vinaambatanishwa pia na mambo hayo mawili. Mfungaji anafungua kwavyo. Miongoni mwavyo ni kama vile sindano za lishe. Kwa sababu inamtosheleza mtu kutokamana na chakula. Vivyo hivyo sindano za kutiwa damu zinamfunguza mfungaji. Kwa sababu damu ni nembo ya chakula na kinywaji. Hata hivyo mara nyingi mtu ambaye anahitaji sindano za lishe au kudungwa sindano za kutiwa damu hurusiwa kula.

Kuhusu sindano za kawaida kwa ajili ya kuzuia magonjwa hazimfunguzi mfungaji. Ni mamoja sindano hizo zinadungwa kwenye misuli au mishipa. Kwa sababu sio kula wala kunywa wala hazileti maana ya hayo mawili. Lakini salama zaidi kwa mfungaji ni yeye acheleweshe kufanya hivo mpaka wakati wa usiku kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya ´ibaadah hii na kutoka nje ya tofauti za wanazuoni wengi wenye kuona kuwa zinafunguza. Hoja yao ni kwamba zinafika tumboni na pia kwa sababu ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kiache chenye kukutia shaka na badala yake kiendee kisichokutia shaka.”[1]

[1] at-Tirmidhiy (2518) na an-Nasaa´iy (5711). at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 18/04/2023