14. Hapo ndipo nuru ya imani huondoka kwa mtu

65 – ´Iysaa bin Yuunus ametuhadithia, kutoka kwa al-Awzaa´iy, kutoka kwa Yahyaa bin Abiy ´Amr as-Saybaaniy ambaye ameeleza kuwa Hudhayfah amesema:

“Mimi nawajua watu wa dini mbili ambao wote wako Motoni. Wafuasi wa dini ya kwanza wanasema kuwa imani ni maneno pasi na matendo, hata kama mtu ataua na kuzini. Wafuasi wa dini nyingine wanasema: “Watangu wetu walikuwa wakituamrisha kuswali swalah tano kila siku, lakini hapana vyengine ni swalah mbili tu: ´Ishaa na Fajr.”

66 – Abu Khaalid al-Ahmar ametuhadithia, kutoka kwa Ibn ´Ajlaan, kutoka kwa ´Abdullaah bin Diynaar, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani ni tanzu sitini au sabini au moja kati ya idadi hizo mbili. Ya juu yake kabisa ni “Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” na ya chini yake kabisa ni kuondosha kitu cha madhara njiani. Hayaa ni tanzu katika imani.”[1]

67 – Ibn ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa az-Zuhriy, kutoka kwa Saalim, kutoka kwa baba yake ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hayaa ni katika imani.”[2]

68 – Wakiy´ ametuhadithia: al-A´mash ametueleza, kutoka kwa Salamah bin Kuhayl, kutoka kwa Habbah al-´Uraniy aliyesema:

“Tulikuwa pamoja na Salmaan wakati ambapo tumesimama uso kwa uso na adui. Akasema: “Hawa ni waumini, hawa ni wanafiki na hawa ni washirikina. Allaah anawanusuru wanafiki kwa du´aa ya waumini, na Allaah akawatia nguvu waumini kwa nguvu ya wanafiki.”[3]

69 – ´Abdah bin Sulaymaan ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Abu Ishaaq, kutoka kwa Abu Qurrah ambaye ameeleza kwamba Salmaan alisema kumwambia bwana mmoja maneno mfano wa:

“Lau utakatwa viungo vyako vya mwili, basi hutoifikia imani.”

70 – Hammaad bin Ma´qal ametuhadithia, kutoka kwa Ghaalib, kutoka kwa Bakr ambaye amesema:

“Lau ningeulizwa kuhusu mtu mbora wa msikitini na kama nashuhudia ya kwamba ni muumini na mwenye imani kamilifu na yuko mbali na unafiki, nisingeshuhudia. Kwa sababu ningeshuhudia jambo hilo, basi ningeshuhudia pia kwamba yuko Peponi. Na ningeulizwa kuhusu mtu muovu kabisa au mchafu kabisa – shaka ni ya Abul-´Alaa´ – na kama nashuhudia ya kwamba ni mnafiki na mwenye unafiki uliokamilika na yuko mbali na imani, nisingeshuhudia. Kwa sababu ningeshuhudia jambo hilo, basi ningeshuhudia pia kwamba yuko Motoni.”

71 – ´Abdullaah bin Numayr ametuhadithia: Fudhwayl bin Ghazwaan ametueleza: ´Uthmaan bin Abiy Swafiyyah al-Answaariy[4]  ametueleza:

“´Abdullaah bin ´Abbaas alisema kuwaambia watumwa wake, mmoja baada ya mwingine: “Nisikuozeshe? Hakuna mtumwa anayezini isipokuwa Allaah huondoa moyoni mwake nuru ya imani.”

[1] Swahiyh. Cheni ya wapokezi nzuri. Muslim ameipokea kupitia kwa Suhayl, kutoka kwa ´Abdullaah bin Diynaar kwa tamko lisemalo:

“Imani ni tanzu sabini, au sitini na kitu. Ya juu yake ni “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” na ya chini yake ni kuondosha chenye kuudhi njiani. Hayaa pia ni tanzu katika imani.”

al-Bukhaariy ameipokea kwa kifupi na yeye ndiye amepokea jumla ya mwisho ya Hadiyth.

[2] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim. Wote wawili wameipokea.

[3] Cheni ya wapokezi ni nzuri. Wapokezi wake ni waaminifu na ni wanamme wa al-Bukhaariy na Muslim – isipokuwa tu al-´Uraaniy, ambaye alikuwa mkweli lakini anakosea. Alikuwa mwenye kuchupa mipaka katika Tashayyu´, kama ilivyo katika “at-Taqriyb”.

[4] Simjui huyu ´Uthmaan bin Abiy Swafiyyah. Hata hivyo si yeye pekee aliyepokea haya. Mtunzi ameitaja huko mbele (94) kwa cheni ya wapokezi nzuri.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 30-32
  • Imechapishwa: 11/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy