13. Asubuhi hali ya kuwa ni muumini, jioni hali ya kuwa kafiri

58 – Ghundur ametuhadithia, kutoka kwa Shu´bah, kutoka kwa al-Hakam bin ´Utaybah: Nimemsikia Ibn Abiy Laylaa akisema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba du´aa hii:

يا مقلب القلوب ثبت قلبي على دينك

“Ee mwenye kuzigeuza nyoyo! Uthibitishe moyo wangu juu ya dini Yako.”

59 – Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Dharr, kutoka kwa Waa-il bin Muhaanah: ´Abdullaah amesema:

“Sijaona walio dini na maoni pungufu wanaomghalibu mwanaume mwenye busara kama nyinyi [wanawake].” Tukasema: “Ni upi upungufu wa akili na dini yetu, ee Abu ´Abdir-Rahmaan?” Akasema: “Ni kule kuacha kwake swalah wakati wa hedhi yake.” Wakasema: “Ni upi upungufu wa akili yake?” Akasema: “Ushahidi wa wanawake wawili ni sawa na ushahidi wa mwanamme mmoja.”

60 – Abu Usaamah ametuhadithia, kutoka kwa al-Hasan bin ´Ayyaash, kutoka kwa Mughiyrah ambaye amesema:

“Ibraahiym aliulizwa kuhusu mtu ambaye anamuuliza mwingine kama ni muumini. Akajibu: “Jibu juu ya hilo ni uzushi. Hata hivyo hainifurahishi kutilia shaka.”

61 – Abu Usaamah ametuhadithia, kutoka kwa Habiyb bin ash-Shahiyd, kutoka kwa ´Atwaa’, kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema:

“Hazini mwenye kuzini pale anapozini hali ya kuwa ni muumini, haibi hali ya kuwa ni muumini na wala hanywi pombe hali ya kuwa ni muumini.”[1]

62 – Abu Khaalid al-Ahmar ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa ´Amaarah bin ´Umayr, kutoka kwa Abu ´Ammaar, kutoka kwa Hudhayfah ambaye amesema:

“Naapa kwa Allaah! Mtu anaweza kuamka akiwa anaona kisha ikaingia jioni na haoni kwa kope.”[2]

63 – Ibn Idriys ametuhadithia, kutoka kwa Muhammad bin Ishaaq, kutoka kwa Sa´iyd bin Yasaar ambaye ameeleza:

“´Umar alifikiwa na khabari ya kuwa kuna bwana mmoja Shaam anayedai kuwa ni muumini. ´Umar akaandika: “Mwagizeni kwangu.” Akafika kwa ´Umar, akamuuliza: “Wewe ndiye ambaye unadai kuwa ni muumini?” Akasema: “Je, watu katika kipindi cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa kitu kingine kama si makundi matatu: muumini, kafiri na mnafiki?” Mimi sio kafiri wala mnafiki.” ´Umar akasema: “Nipe mkono.” Ibn Idriys akasema: “Alisema hivo kwa sababu aliridhia alichokisema.”[3]

64 – Shabaabah bin Sawwaar ametuhadithia: Layth bin Sa´d ametueleza, kutoka kwa Yaziyd, kutoka kwa Sa´d bin Sinaan, kutoka kwa Anas, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Kabla ya kufika Saa kutakuwa na mitihani kama kipande cha usiku wenye giza. Mtu atarauka hali ya kuwa ni muumini na ifike jioni hali ya kuwa ni kafiri, au arauke hali ya kuwa ni kafiri na ifike jioni hali ya kuwa ni muumini.”[4]

[1] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Imekwishatangulia kwa njia nyingine kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[2] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Abu ´Ammaar alikuwa anaitwa ´Ariyb bin Humayd ad-Duhniy.

[3] Muhammad bin Ishaaq bin Yasaar, mtunzi wa wasifu wa Mtume. Alikuwa mwaminifu, lakini pia mudallis. Alikuwa haweki wazi amesikia kutoka kwa nani.

[4] Swahiyh. Cheni ya wapokezi ni nzuri. Itakuja huko mbele iliyosimuliwa na Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) kwa nambari 83.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 11/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy