Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Ama kujinasibisha kwa imaam fulani katika vitaga vya dini, kama mfano wa madhehebu manne, ni jambo lisilosemwa vibaya. Tofauti katika matawi ni rehema na wanaotofautiana ni wenye kusifiwa kwa kutofautiana kwao na wanapewa thawabu kwa Ijtihaad zao. Tofauti yao ni rehema kunjufu na kukubaliana kwao [juu ya jambo fulani] ni hoja imara.

Tunamwomba Allaah atukinge na Bid´ah na fitina, atufufue na Uislamu na Sunnah, atujaalie ni miongoni mwa wenye kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika maisha haya na atukusanye na kundi lake baada ya kufa kwetu kwa rehema na fadhila Zake. Aamiyn.

Hapa ndipo mwisho wa ´Aqiydah. Himdi zote ni Zake Allaah Mmoja. Swalah na amani zimwendee bwana wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

MAELEZO

Maana ya vitaga au matawi ni yale yanayojengwa juu ya kitu kingine. Maana ya istilahi ni yale yasiyohusiana na ´Aqiydah kama mfano wa mambo yanayohusu twahara, swalah na mfano wake. Kutofautiana kwayo si jambo la kusimangwa muda wa kuwa yanatokana na nia safi na ijtihaad na si kwamba yametokana na matamanio na ushabiki. Mambo kama hayo yametokea katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala hakuwakemea. Aliwahi kusema katika vita vya Banuu Quraydhwah:

“Asiswali mmoja wenu ´Aswr isipokuwa kwa Banuu Quraydhwah.”

Muda wa swalah ukafika kabla ya kufika wanakoenda ambapo baadhi yao wakachelewesha swalah mpaka walipofika Banuu Quraydhwah na wengine wakaswali wakati walipochelea kumalizika muda wa swalah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumkaripia yeyote katika wao.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy.

Tofauti katika mambo hayo imepatikana kwa Maswahabah ambao ndio karne bora. Isitoshe kitu hicho hakipelekei katika uadui, chuki na wala haufarikishi umoja tofauti na inavokuwa makinzano kuhusu mambo ya msingi.

[1] al-Bukhaariy (946).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 163-164
  • Imechapishwa: 22/02/2023