130. ´Aqiydah ya wanazuoni wa ulimwenguni kote

26 – Muhammad bin al-Hasan (131-189), mwanachuoni wa ´Iraaq katika Hadiyth.

163 – Ahmad bin al-Qaasim bin ´Atwiyyah amesema: Nimemsikia Abu Sulaymaan al-Juujaaniy: Nimemsikia Muhammad bin al-Hasan amesema:

”Naapa kwa Allaah! Siswali nyuma ya anayesema kuwa Qur-aan ni kiumbe. Hakuna aliyeniomba fatwa juu ya hilo isipokuwa nilimwamrisha kuirudia swalah yake.”[1]

164 – Mtunzi amesimulia kutoka kwa ´Amr bin Wahb: Nimemsikia Shaddaad bin Hakiym akisema:

”Muhammad bin al-Hasan amesema kuhusu Hadiyth mfano wa ”Allaah hushuka katika mbingu ya chini”: ”Hadiyth hizi zimepokelewa na watu wenye kuaminika. Tunazisimulia, tunaziamini na hatuzifasiri.”[2]

165 – Abul-Qaasim Hibatullaah al-Laalakaa’iy, Shaykh Muwaffaq-ud-Diyn al-Maqdisiy na wengine wamesimulia kutoka kwa ´Abdullaah bin Abiy Haniyfah ad-Dawsiy, ambaye amesema: Nimemsikia Muhammad bin al-Hasan akisema:

“Wanazuoni wote Mashariki na Magharibi wameafikiana juu ya kuamini Qur-aan na Sunnah zilizopokelewa na wapokezi wenye kuaminika kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu sifa za Mola (´Azza wa Jall) pasi na tafsiri[3], kuzielezea wala kuzifananisha. Yule mwenye kufasiri kitu katika hayo basi ametoka katika yale aliyokuwemo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na amefarikiana na mkusanyiko. Kwani wao hawakueleza na wala hawakufasiri. Lakini waliyaamini yaliyomo ndani ya Qur-aan na Sunnah kisha wakanyamaza. Yule mwenye kusema yale yaliyosemwa na Jahm basi amefarikiana na mkusanyiko. Kwa sababu amemweleza kwa sifa isiyokuwa chochote.”[4]

[1] Simjui ni nani Abu Sulaymaan al-Juujaaniy.

[2] al-Laalakaa’iy (2/433) ambayo cheni yake ya wapokezi imesimuliwa na mtunzi. Ikiwa ´Amr bin Wahb ni at-Twaa-ifiy, hali yake haitambuliki.  Na kama alikuwa ni al-Qurashiy, Ibn Abiy Haatim amesimulia kutoka kwa baba yake, ambaye amesema:

“Ni mwenye kusimulia Hadiyth zinazotofautiana.” (al-Jarh wat-Ta´diyl (3/1/266))

[3] Ibn Taymiyyah amesema:

”Anachokusudia kwa ”pasi na tafsiri” ni zile tafsiri za Jahmiyyah wakanushaji ambao wamezusha tafsiri ya sifa za Allaah kwa njia inayotofautiana na tafsiri ya Maswahabah na wanafunzi wao.” (al-Hamawiyyah, uk. 115)

[4] Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Taymiyyah katika “Majmuu´-ul-Fataawaa” (4/4-5).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Uluww lil-´Aliy al-Ghaffaar, uk. 152-153
  • Imechapishwa: 22/07/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy