13. Ujumbe wa Muhammad unatosheleza

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema wakati alipokuwa anathibitisha msingi huu:

“Ujumbe wake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wenye kutosheleza, wenye kuenea na kwa walimwengu wote na haukuacha haja ya kitu chochote. Haitimii imani ya yeyote isipokuwa kwa kuthibitisha kuenea kwa Ujumbe wake… Hakuna yeyote katika watu wazima anayetoka nje ya Ujumbe wake. Hakuna aina yoyote ya haki ambayo Ummah wanaihitaji katika elimu na matendo yake eti yakakosekana katika Ujumbe wake.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekufa na hakuna ndege yeyote anayeruka kwa mbawa zake angani isipokuwa amewatajiaUmmah elimu yake. Amewafunza kila kitu, kukiwemo ada za kukidhi haja, adabu za jimaa, za jimaa, kusimama, za kukaa, za kula, za kunywa, za kupanda, za kushuka, za safari, za uenyeji, za kunyamza, za kuongea, za kujitenga, za kuchanganyika, za utajiri, za umasikini, za uzima, za maradhi na nyingine zote za uhai na za kifo.

Amewasifia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ´Arshiy na Kursiy, Malaika na majini, Moto na Pepo, siku ya Qiyaamah na yanayohusiana nayo, mpaka kana kwamba mtu anaiona kwa macho.

Amewatambulisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Mungu wao anayeabudiwa kwa njia kamilifu, na kwamba wanamuona kwa sifa Zake kamilifu zaidi na za utukufu.

Amewatambulisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Mitume na nyumati zao na yale yote yaliyowapitikia, kama kwamba walikuwa kati yao.

Amewatambulisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yale yote yanayopelekea katika kheri na shari, kidogo chake na kikubwa chake, kwa njia ambayo haikufanywa na Mtume yeyote kwa Ummah wake hapo kabla.

Amewatambulisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali za kifo na zile neema na adhabu zinazopitikia kiwiliwili na roho ndani ya kaburi, kwa njia ambayo haikufanywa na Mtume yeyote kwa Ummah wake hapo kabla.

Amewatambulisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yote yanayojulisha Tawhiyd, utume na kufufuliwa na kuyarudi mapote yote ya ukafiri na upotofu. Yule anayeyajua hayo hana haja ya kitu kingine baada yake isipokuwa ambaye atamfikishia mambo hayo, kumbainishia na kumuwekea wazi yale yaliyofichikana kwake.

Amewatambulisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mbinu za vita, makabiliano na adui, njia zote za nusura na ushindi kwa upeo ambao, endapo wangeyatambua, wakayaelewa na kuyatilia umuhimu ipasavyo, basi hakuna kabisa adui yeyote ambaye angethubutu kusimama dhidi yao.

Amewatambulisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vitimbi vya Ibliys na mbinu zake anazotumia vibaya kuwaendea, pamoja na namna ya kujilinda na njama, vitimbi na shari zake.

Amewatambulisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya nafsi zao, sifa zake, vitimbi vyake na siri zilizojificha, kwa njia ya kwamba hawana haja ya kitu kingine zaidi.

Amewatambulisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mambo yanayohusu utafutaji wa riziki zao kwa njia ya kwamba, endapo wangelizijua na wakazitendea kazi, basi yangelinyooka maisha yao kwa njia nzuri kabisa.

Kwa kufupisha ni kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewajia na kheri zote za duniani na Aakhirah. Allaah hawakufanya wakamuhitajia mwingine zaidi yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[1]

[1]I´laam-ul-Muwaqqi´iyn (4/375-376).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 07/05/2023