13. Sura ya nne: Ubainifu wa mfumo wa Qur-aan katika kuthibitisha upwekekaji wa Allaah katika uumbaji, riziki na mengineyo

Mwenendo wa Qur-aan katika kuthibitisha uwepo wa muumbaji na umoja Wake ni mfumo unaoenda pamoja na maumbile yaliyonyooka na akili timamu. Hayo ni kwa kusimamisha hoja sahihi zinazokinaisha na akili na wakajisalimisha kwazo mahasimu. Miongoni mwazo:

1- Ni jambo linalojulikana fika ya kwamba chenye kuzuka ni lazima kiwe na ambaye kakifanya kuzuka

Suala hili ni la kilazima na linalojulikana kimaumbile mpaka kwa watoto. Lau mtu atampiga mtoto ambaye amezubaa na asimuone na akauliza ni nani aliyempiga, akiambiwa kwamba hakuna yeyote aliyempiga basi akili yake haitokubali eti kipigo hicho kimejitokeza hivi burebure. Akiambiwa kuwa fulani ndiye kampiga basi atalia mpaka na yeye ampige. Kwa ajili hiyo amesema (Ta´ala):

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaj?”[1]

Allaah ameuliza kwa njia ya uulizaji wa kupinga ili abainishe kuwa matangulizi haya yanatambulika fika na hayawezi kukanushwa. Amesema:

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote… “

Bi maana pasi na muumbaji aliyewaumba au wamejiumba wao wenyewe? Yote mawili ni batili. Kwa hivyo imelazimika kwamba kuna muumbaji aliyewaumba. Naye si mwengine ni Allaah (Subhaanah). Hakuna muumbaji mwengine zaidi Yake. Amesema (Ta´ala):

هَـٰذَا خَلْقُ اللَّـهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ

”Huu ni uumbaji wa Allaah, basi nionyesheni ni kitu gani walichokiumba wasiokuwa Yeye.”[2]

أَرَأَيْتُم مَّا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَرُونِي مَاذَا خَلَقُوا مِنَ الْأَرْضِ

”Je, mnaonaje wale mnaowaomba badala ya Allaah! Nionyesheni nini wameumba katika ardhi.”[3]

وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَا يَخْلُقُونَ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ

”Wale wanaowaomba badala ya Allaah hawaumbi kitu chochote, bali wao wanaumbwa.”[4]

أَفَمَن يَخْلُقُ كَمَن لَّا يَخْلُقُ ۗ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ

”Je, [Allaah] anayeumba ni sawa kama asiyeumba? Je, kwa nini hamkumbuki?”[5]

Pamoja na changamoto hizi zilizokariri hakuna yeyote aliyedai kwamba ameumba kitu japo madai peke yake sembuse kuthibitisha jambo hilo. Kwa hivyo imebaini kuwa Allaah (Subhaanah) ndiye muumbaji hali ya kuwa peke yake hana mshirika.

[1] 52:35

[2] 31:11

[3] 46:04

[4] 16:20

[5] 16:17

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 33-34
  • Imechapishwa: 05/02/2020