14. Sura ya nne: Dalili ya pili inayothibitisha juu ya upwekekaji wa Allaah katika uumbaji, riziki na mengineyo II

2- Mpangilio wa ulimwengu na ilivyo vizuri ni dalili tosha inayothibitisha kwamba mwendeshaji na Mungu wake ni mmoja na Mola mmoja  hali ya kuwa peke yake hana mshirika bila kipingamizi. Amesema (Ta´ala):

مَا اتَّخَذَ اللَّـهُ مِن وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَـٰهٍ ۚ إِذًا لَّذَهَبَ كُلُّ إِلَـٰهٍ بِمَا خَلَقَ وَلَعَلَا بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ

“Allaah hakujichukulia mwana yeyote na wala hakukuwa pamoja Naye mwabudiwa yeyote, hapo bila shaka kila mwabudiwa angelichukua vile alivyoviumba na bila shaka baadhi yao wangeliwashinda wengineo.”[1]

Mungu wa haki ni lazima awe muumbaji mtendaji. Lau Yeye (Subhaanah) angelikuwa na mungu mwengine anayeshirikiana naye katika ufalme Wake – Allaah ametakasika kutokamana na hayo – basi mungu mwengine huyo angelikuwa na uumbaji na utendaji. Hivyo asingeliridhia ushirika wa huyo mungu mwengine. Bali akiweza kumshinda huyo mshirika wake na akapwekeka na ufalme wake na uungu wake pasi naye angelifanya. Asipoweza kuyafanya hayo basi angelipwekeka kwa fungu lake katika ufalme na uumbaji. Mambo ni kama wanavyopwekeka wafalme wa duniani wao kwa wao kwa ufalme wao. Matokeo yake kunatokea mgawanyiko. Kwa hivyo ni lazima kupatikane moja katika mambo matatu

a) Ima mmoja amshinde mwengine na apwekeke na ufalme pasi na mwengine.

b) Ima kila mmoja katika wao apwekeke kutokamana na mwengine kwa ufalme na uumbaji wake. Matokeo yake kutokee mgawanyiko

c) Ima awe chini ya mfalme mmoja ambaye atamwendesha atakavyo. Hivyo yeye huyo ndiye awe mungu wa haki na wengine wawe ni waja wake. Huu ndio uhakika wa mambo. Katika ulimwengu hakukutokea mgawanyiko wala kasoro. Hayo yanafahamisha kuwa mwendeshaji ni mmoja, asiyekuwa na mkinzani, na kwamba mfalme wake ni mmoja, asiyekuwa na mshirika.

[1] 23:91

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 05/02/2020