8 – Maji yawe masafi na yenye kuruhusiwa/ya halali

Sharti ya nane miongoni mwa sharti za kusihi kwa wudhuu´ ni maji yawe masafi. Mtu akitawadha kwa maji yenye najisi basi wudhuu´ wake hautosihi. Kwani maji yenye najisi hayaondoshi hadathi. Maneno yake mtunzi:

“Maji yawe yenye kuruhusiwa/ya halali.”

yana maana kwamba yawe ya halali na yenye kuruhusiwa. Endapo mtu atatawadha kwa maji aliyopokonya, basi mtunzi (Rahimahu Allaah) ameonelea – na ndio madhehebu ya Hanaabilah[1] – kwamba wudhuu´ hausihi. Maji ni masafi na hayana najisi lakini hata hivyo kitendo cha kuyapora ndio ni haramu na hakiruhusiwi. Hivyo wudhuu´ wake hausihi. Wako wanachuoni wengine wenye kuona kuwa wudhuu´ wake unasihi licha ya kuwa anapata dhambi. Anapata thawabu juu ya wudhuu´ na swalah lakini anapata dhambi za uporaji.  Tukitazama upande wa kwamba maji yameporwa anapata dhambi. Tukitazama upande wa kwamba ametawadha kwa maji masafi basi wudhuu´ wake umesihi[2]. Tofauti hii ni kama ya kusihi kwa swalah iliyoswaliwa katika ardhi iliyoporwa[3].

9 – Kuondosha kila kinachozuia maji kufika kwenye ngozi

Sharti ya tisa miongoni mwa sharti za kusihi kwa wudhuu´ ni Kuondosha kila kinachozuia maji kufika kwenye ngozi kama mfano wa mkandaji unga. Ni lazima aondoshe unga huo. Vivyo hivyo rangi inayopakwa kwenye kucha na baadhi ya wanawake na inazuia maji. Ni lazima aiondoshe kabla ya kuanza kutawadha. Asipoiondosha basi wudhuu´ wake hausihi. Kwa sababu kutabaki maeneo ambayo hayafikiwi na maji.

Kuhusu hina na mafuta hayazuii maji kufika kwenye ngozi.

10 – Kuingia kwa wakati wa kile kitendo cha faradhi kwa yule ambaye daima yuko katika hali ya hadathi

Sharti ya tisa miongoni mwa sharti za kusihi kwa wudhuu´ ni Kuingia kwa wakati wa kile kitendo cha faradhi kwa yule ambaye daima yuko katika hali ya hadathi. Ambaye hadathi yake ni ya nyakati zote basi wudhuu´ wake hausihi mpaka uingie wakati wa swalah. Ambaye yuko na hadathi wakati wote, kama mfano kutokwa hovyo na mkojo masaa ishirini na nne, huyu anaswali kwa hali yake. Ataweka kwenye uume wake kitambara na baada ya hapo ataosha yale maeneo yaliyopatwa na mkojo. Asitawadhe isipokuwa baada ya kuingia wakati wa kila swalah. Baada ya hapo ataswali hata kama atatokwa kwenye uume wake na mkojo kidogo. Kwani mtu kama huyu hana namna nyingine kwa sababu hadathi yake ni ya nyakati zote. Lakini kama kuna nyakati ambapo hadath inasita, basi atachungana na wakati huo ambapo atatawadha na kuswali hata kama atapitwa na swalah ya mkusanyiko. Kwa sababu swalah ya mkusanyiko ni lazima. Lakini wudhuu´ ni sharti ya kusihi kwa swalah. Aidha sharti ni yenye kupewa kipaumbele kabla ya jambo la lazima.

Mfano mwingine wa ambaye hadathi yake inakuwa nyakati zote ni mwanamke ambaye anatokwa na damu ya ugonjwa. Huyu ana hukumu moja kama ambaye anatokwatokwa na mkojo wakati wote. Mwanamke huyu anatakiwa kujisitiri na atawadhe pindi kunapoingia muda wa kila swalah. Mfano mwingine ni wa yule ambaye ana donda endelevu[4].

Msimamo ambao unatolewa fatwa na ulio salama zaidi juu ya dini ya muislamu ni kwamba yule ambaye hadathi yake ni ya nyakati zote, basi anatakiwa kutawadha kunapoingia muda wa kila swalah. Asiswali faradhi mbili kwa wudhuu´ mmoja. Akisema kuwa hakutokwa na kitu, tutamwambia kwamba yeye hadathi yake ni ya nyakati zote na kwamba ni mwenye kupewa udhuru na kwamba atawadhe kunapoingia wakati wa kila swalah.

[1] al-Mardaawiy amesema:

”Ama kutawadha kwa maji yaliyoporwa, maoni sahihi ya madhehebu [ya Hanaabilah] ni kwamba twahara yake haisihi kwayo. Haya ni miongoni wa yale mambo ambayo madhehebu [ya Hanaabilah] wamepwekeka nayo. Kuna maoni mengine yamepokelewa kutoka kwake [Imaam Ahmad bin Hanbal] kwamba inasihi lakini hata hivyo akachukiza jambo hilo.” (al-Inswaaf (01/28-29)).

[2] Tazama ”al-Majmuu´” (02/284).

[3] Tazama ”Jaamiy´-´Uluum wal-Hikam”, uk. 61 ya Ibn Rajab.

[4] Tazama ”al-Mughniy” (01/206) ya Ibn Qudaamah.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 09/12/2021