Miongoni mwa sababu familia kupata furaha ni mwanaume ashikamane na mfumo wa wema katika namna ya kutaamiliana na familia yake. Lengo ni ili awe na historia yenye kusifiwa, awe ni mwenye dhamira nzuri, awe mwepesi, awe na kirafiki na mkewe na watoto wake, mwenye kuwaonea huruma na awaonee huruma. Upole hauwi kwenye kitu isipokuwa hukipamba na hauondolewi kwenye kitu isipokuwa hukifanya kibaya[1]. Mume hawakalifishi kwa kitu wasichokiweza na ajizoweze kuyakubali yale mapungufu yao yasiyompendeza. Akiona kitu kutoka kwa mke wake asichokipenda ajikumbushe uzuri wake. Akiona kosa kutoka kwa mtoto wake ajikumbushe ile kheri inayopatikana kwa mtoto wake huyo. Kwa njia hiyo yeye na familia yake wote wawili watakuwa na furaha. Mume anatakiwa kutambua kuwa mwanamke ni kiumbe dhaifu na atambue kuwa amemchukua kwa amana ya Allaah na hivyo asimdhulumu hata siku moja. Anatakiwa kumsitiri mwanamke na wala asieneze siri zake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Katika watu wataokuwa na ngazi mbaya kabisa siku ya Qiyaamah ni mwanaume anayemwingilia mwanamke na mwanamke akamwingilia halafu akaeneza siri zake.” Muslim (1437).

Huyu ndiye mtu ambaye yuko na ngazi mbaya kabisa siku ya Qiyaamah. Mwanaume anayefuata mfumo wa wema anamchekesha mke wake na kucheza naye. Yote hayo kwa ajili ya kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anatakiwa pia kuwachunga kwa sababu yeye ndiye mchungaji. Asimpige mke wake kipigo kikubwa na cha kuumiza. Ikibidi kumpiga basi anampiga tu kipigo cha kumtia adabu kiasi cha kwamba mwanamke ahisi kuwa anamtia adabu. Ama ikiwa atampiga kipigo cha kumuumiza na akampa kipigo kweli kweli na juu yake akamwongezea bakora kutakosekana furaha nyumbani. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mmoja wenu asimpige mke wake kama anavyopigwa mtumwa halafu akataka kumjamii mwisho wa siku.” al-Bukhaariy (5204).

Akimchapa bakora atachoshwa naye na hatokuwa na furaha naye.

Mwanaume anayepita juu ya mfumo wa wema nyumbani kwake anampa mwanamke haki zake alizopewa na Allaah. Isitoshe hamtuhumu, hamkebehi, hawakebehi familia yake, hamlaani na hawalaani familia yake. Kwa nini? Anatambua ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa: “Ni ipi haki ya mmoja katika wake zetu juu yetu?” Akajibu kwa kusema: “Amlishe pindi atapokula, amvishe pindi atapovaa, asipige uso wake, asimkebehi na wala asimhame isipokuwa tu nyumbani.” Abu Daawuud (2142), Ibn Maajah (1850), Ibn Hibbaan (09/4175), al-Haakim (02/2764), Ahmad (04/446 na 447) na (05/03 na 5). Mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim ambapo adh-Dhahabiy ameafikiana naye na al-Albaaniy katika “al-Irwaa´” (2033).

Hamchukulii mke wake katika kila kitu. Kwa kuwa anatambua kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nakuusieni kuwatendea wanawake wema. Hakika mwanamke ameumbwa kwa ubavu uliyopinda. Sehemu iliyopinda zaidi ni ile ya juu. Ukitaka kuinyoosha utaivunja na ukiiacha kabisa itaendelea kuwa imepinda. Nakuusieni kuwatendea wanawake wema.” al-Bukhaariy (3331), Muslim (1468) na matamshi ni yake.

Mwanaume akishikamana barabara na mfumo wa wema basi itapatikana furaha nyumbani kwake na kutapatikana kheri nyingi katika familia hii. Kadhalika mwanamke anatakiwa katika ujumba wake kupita katika mfumo wa wanawake wema. Anatakiwa kuadhimisha haki za mume wake na familia yake. Kwa kuwa anatambua kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameikuza haki ya mume wake juu yake. Huu ni mlango mpana ambao nimeuzungumzia kwenye muhadhara uliochapishwa kwa kichwa cha khabari “Haqq-uz-Zawjayn”. Katika muhadhara huo nimetaja yaliyothibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika haki za mume na mke. Hapana shaka lau haki hizi zilizothibiti katika Sunnah zingelitendewa kazi basi hiyo ingelikuwa ni sababu kubwa miongoni mwa sababu zinazofanya familia kupata furaha.

[1] Muslim (2594).

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Asbaab sa´aadat-il-Usrah, uk. 41-44
  • Imechapishwa: 14/10/2016