Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Allaah alimtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa uongofu na dini ya haki ili awaondoshe watu kutoka kwenye giza na kuwaingiza katika nuru. Amethibitisha kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemtuma hali ya kuwa ni mwenye kulingania Kwake kwa idhini Yake na taa lenye kuangaza. Alimwamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aseme:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata.”[1]

MAELEZO

Baada ya Shaykh (Rahimahu Allaah) kusema kuwa anasema yale yaliyosemwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wale waliotangulia awali ambao ni Muhaajiruun na Answaar, maimamu waliowafata kwa wema, akatoa sababu kwa kusema kuwa Allaah amemtuma Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa uongofu na dini ya haki. Kwa hivyo miongoni mwa uongofu na dini ya haki vinavyochukua nafasi ya mbele kunaingia pia majina na sifa za Allaah. Uongofu ni elimu yenye manufaa na dini ya haki ni matendo mema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumilizwa kwa mambo mawili; elimu yenye manufaa na matendo mema. Miongoni mwa elimu yenye manufaa na matendo mema ni kuyaamini majina na sifa za Allaah ndani ya Qur-aan na Sunnah kwa mujibu wa uelewa wa wale waislamu wa mwanzo. Maudhui haya hayakuwatatiza, hawakuongea pasi na dalili. Bali walilikubali jambo hilo kwa kujisalimisha na kuyanyenyekea matamshi na maana, jambo ambalo ndio haki. Huu ndio uongofu na dini ya haki. Yule anayekwenda kinyume nayo ameenda kinyume na yale aliyotumilizwa nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu msingi wa elimu zote ni kuwa na utambuzi juu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), majina, sifa Zake na zile ´ibaadah anazostahiki:

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

“Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako.”[2]

Kuwa na utambuzi juu ya ´Aqiydah sahihi ndio msingi, kwa msemo mwingine kuwa na utambuzi juu ya hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Linatakiwa kuaminiwa kimatamshi, maana, kuliitakidi na yote yanayoipelekea. Huu ndio msingi wa dini na imani. Huu ndio msingi wa nyujumbe zote za Mitume:

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.””[3]

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[4]

Hiki ndio kiini cha nyujumbe na inahusiana na kuihakikisha haki ya Allaah (´Azza wa Jall) ya kuabudiwa. Hili haliwezi kuhakikiwa isipokuwa kwa kumtambua Allaah, kwa majina na sifa Zake. Sisi tunamtambua Allaah (´Azza wa Jall) kwa yale aliyotutambulisha juu Yake kupitia majina na sifa Zake zilizotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah. Huu ndio msingi.

[1] 12:108

[2] 47:19

[3] 16:36

[4] 21:25

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 38-39
  • Imechapishwa: 28/07/2024