13. Msimamo wa maimamu wa nne pale maoni yao yatatofautiana na dalili

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

ودنْ بكتابِ الله والسننِ التي

02 – Fuata katika dini yako Kitabu cha Allaah na Sunnah ambazo

أتت عنْ رسول الله تنجو وتربحُ

zimekuja kutoka kwa Mtume wa Allaah utafaulu na kufaidika

MAELEZO

Ifanye dini yako ni yenye kuchukuliwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah ambazo ni zile Hadiyth Swahiyh. Kuhusu yenye kuja kutoka kwa wengine yanatakiwa kuangaliwa vyema. Endapo yatakuwa ni yenye kuafikiana na Qur-aan na Sunnah yatatendewa kazi. Ikiwa yanatofautiana na Qur-aan na Sunnah yatarudishwa kwa mwenye nayo. Maimamu wanausia kufanya hivi. Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Maoni yangu yakitofautiana na maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam),  basi yachukueni maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yatupeni maoni yangu kando.”[1]

Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kila mmoja wetu ni mwenye kurudi na kurudiwa isipokuwa bwana mwenye kaburi hili.”

Bi maana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa kuwa alikuwa akifunza katika msikiti wake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) harudiwi kabisa. Maneno yake (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) yanakubaliwa. Kuhusu wengine yakiafikiana na Qur-aan na Sunnah yatatendewa kazi, na yakitofautiana nayo yanarudishwa.

Imaam Abu  Haniyfah (Rahimahu Allaah) – naye ndiye wa kwanza katika maimamu wanne – amesema:

“Ikija Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tutaikubali, ikija Hadiyth kutoka kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tutaikubali na ikija Hadiyth kutoka kwa waliokuja baada ya Maswahabah, wao ni wanaume na sisi pia ni wanaume.”

Bi maana chenye kutoka kwa asiyekuwa Allaah, Mtume Wake na Maswahabah zake kitatakiwa kuangaliwa kwanza hata kama kitakuwa kimetoka kwa mtu aliye bora kabisa. Haijalishi kitu hata kama ni wanafunzi wa Maswahabah. Kitahitaji kuangaliwa; kikiafikiana na Qur-aan na Sunnah kitachukuliwa. Kikienda kinyume navyo kitaachwa.

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ninastaajabishwa na watu wanaojua elimu ya mlolongo wa wapokezi na usahihi wake halafu wanaenda katika maoni ya Sufyaan.”

Sufyaan ath-Thawriy alikuwa ni mwanachuoni na imamu mtukufu.

Akaendelea kusema (Rahimahu Allaah):

“Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije ikawapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.” (24:63)

Haijuzu kuchukua maoni ya mwanachuoni pasi na kujali ni elimu kiasi gani atakuwa amefikia isipokuwa mpaka yawe yamejengwa juu ya dalili sahihi. Ikiwa yanaenda kinyume na dalili, basi haijuzu kuyatendea kazi. Kwa kuwa hakuna maoni ya yeyote ambayo yanaweza kusimama pamoja na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚإِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Enyi mlioamini! Msitangulie mbele ya Allaah na Mtume Wake. Mcheni Allaah, kwani hakika Allaah ni Mwenye kusikia na ni Mjuzi wa kila kitu.” (49:01)

[1] Tazama “Qawaa´id at-Tahdiyth”, uk. 273 ya al-Qaasimiy, “Siyar A´laam-in-Nubalaa” (10/35) na wengineo

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 30/12/2023