12. Misingi ya kujengea dalili na Radd kwa Qur-aaniyyuun

Kila kilichosihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ni wajibu kukichukua, kukifuata na kukitendea kazi. Ni mamoja ikiwa kimepokelewa kwa njia wasimulizi wengi (الحديث المتواتر) au kimepokelewa kwa njia ya msimulizi mmoja (الحديث الآحاد), tofauti na wanavyofanya watu wa Bid´ah ambao wanaikataa Sunnah. Wanasema kuwa Qur-aan inawatosheleza. Ni jambo linalojulikana kwamba ambaye ataitendea kazi Sunnah basi kaitendea kazi vilevile Qur-aan. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

“Yale anayokupeni Mtume yachukueni, na yale anayokukatazeni yaacheni.” (59:07)

Halafu hawa wanasema kuwa Qur-aan inatutosheleza.

Amesema (Jalla wa ´Alaa):

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ

“Atakayemtii Mtume basi amemtii Allaah.” (04:80)

وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ

“Mfuateni ili mpate kuongoka.” (07:158)

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Mtiini Allaah na Mtume mpate kurehemewa.” (03:132)

Watu hawa wanasema uongo pale wanaposema kuwa wanaitendea kazi Qur-aan pekee midhali wameiacha Sunnah.

Jengine ni kwamba Qur-aan imekuja kwa jumla. Sunnah ndio inayoibainishia na kuifafanua. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema kumwambia Mtume Wake:

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao.” (16:44)

Sunnah ndio yenye kuifasiri Qur-aan, kuiweka wazi na kuifahamisha. Sunnah ina mafungamano yenye nguvu kabisa na Qur-aan. Kwa sababu Sunnah ndio yenye kuibainisha, kuiweka wazi, kufafanua yaliyo ya jumla na kuyafunga ambayo yameachiwa. Sivyo tu, bali Qur-aan inaweza kufuta Sunnah na kinyume chake, Qur-aan ikaifuta Qur-aan na Sunnah ikaifuta Sunnah. Ni lazima yapatikane mambo haya makuu. Watu hawa wenye kuipuuza Qur-aan walielezewa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akatahadharisha nao aliposema:

“Kunakaribia kuwepo mtu aliyeshiba aegemee kitandani mwake. Akaelezwa Hadiyth miongoni mwa Hadiyth ambapo atasema: “Baina yetu sisi na nyinyi kuna Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall). Tutayoyatapa humo ya halali na sisi pia tutayahalalisha na tutayoyapata humo ya haramu na sisi pia tutayaharamisha. Tanabahini! Hakika aliyoharamisha Mtume wa Allaah ndio yale yale aliyoharamisha  Allaah.”[1]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimepewa Qur-aan na kitu mfano wake.”

Bi maana Sunnah.

Amesema (Ta´ala):

وَأَنزَلَ اللَّـهُ عَلَيْكَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ

“Allaah amekuteremshia Kitabu na Hekima.” (04:113)

وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ

“Awafunze Kitabu na Hekima.” (03:164)

Kitabu ni Qur-aan na Hekima ni Sunnah. Sunnah ni kitu cha lazima na ndio msingi wa pili miongoni mwa misingi ya kujengea dalili ambayo kuna maafikiano juu yake.

Kuhusu tofauti ya watu hawa haizingatiwi. Kwa sababu watu hawa ima ni Khawaarij, wajinga au wanaojifanya kuwa ni wasomi. Kuna uwezekano vilevile wana malengo mengine wanachotaka ni kuiharibu dini hatua kwa hatua. Tofauti yao haizingatiwi na maneno yao hayaangaliwi. Sunnah sahihi ndio inatakiwa kutendewa kazi, ni mamoja iwe katika mambo ya matawi au ya msingi.

Kadhalika wapuuze wale wenye kusema kuwa mapokezi yaliyopokelewa na msimulizi mmoja yasitendewe kazi katika mambo ya ´Aqiydah. Yanatakiwa kutendewa kazi katika mambo ya matawi peke yake. Wanaonelea kuwa ni dalili zenye kutia mashaka. Tunawaambia: ni zenye kuwatia mashaka nyinyi. Kwa waumini sio dalili zenye kutia mashaka. Ni dalili zinazofidisha yakini. Maadamu zimesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi zinafidisha elimu. Hazitii mashaka. Zinatendewa kazi katika mambo ya ´Aqiydah, biashara na mengineyo.

3 – Msingi wa tatu ni maafikiano. Dalili yake ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, basi Tutamgeuza alikogeukia mwenyewe na tutamuingiza Motoni – ni uovu ulioje mahali pa kuishia!” (04:115)

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ummah wangu hauafikiani juu ya upotevu.”[2]

Maafikiano ya kimaneno ni hoja yenye kukata mashauri. Kuhusu maafikiano ya kunyamazia ni hoja yenye kutia mashaka. Kwa sababu kuna uwezekano kukawepo aliyeonelea kinyume ingawa haikubainika. Lakini wanazuoni wote wakisema neno na wakaafikiana juu yake na pasiwepo ambaye alionelea kinyume, basi hiyo ni hoja yenye kukata mashauri kabisa.

4 – Msingi wa nne ni kipimo (Qiyaas). Ni kunyofoa hukumu kutoka katika msingi kutokana na kasoro iliyopo. Hivi ndivyo wanavyoonelea wanazuoni wengi na Dhwaahiriyyah na baadhi ya Hanaabilah wameonelea kinyume. Lakini wengi katika Ummah wanaonelea kutumia kipimo. Ni dalili sahihi endapo itatimiza masharti yaliyotajwa katika vitabu vya misingi.

Mbali na hizo kumebaki misingi mingine kadhaa kama mfano wa maneno ya Swahabah n.k. Mambo haya wanazuoni wametofautiana juu yake na ni tofauti iliyo na nguvu. Kuhusu tofauti iliyopo juu ya kipimo haina nguvu. Wengi wanaonele kutumia kipimo. Imaam Ahmad amesema:

“Kipimo kinatumiwa wakati wa dharurah.”[3]

Ni kama mfano wa nyamafu inaliwa wakati wa dharurah. Kunapokuwepo dalili katika Qur-aan na Sunnah hakuna haja ya kipimo. Isipopatikana ndio kipimo kinaendewa kwa sababu ya dharurah.

[1] Abu Daawuud (4604), at-Tirmidhiy (2664), Ibn Maajah (12), Ahmad (04/131) na wengine

[2] Abu Daawuud (4253), at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” (3440) na wengineo

[3] adh-Dhahabiy katika “as-Siyar” (10/77)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 59-62
  • Imechapishwa: 17/12/2023