Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

ودنْ بكتابِ الله والسننِ التي

Fuata katika dini yako Kitabu cha Allaah na Sunnah ambazo

أتت عنْ رسول الله تنجو وتربحُ

 zimekuja kutoka kwa Mtume wa Allaah utafaulu na kufaidika

MAELEZO

Fuata Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ifanye dini yako ni yenye kuchukuliwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah, na isiwe yenye kutoka katika matamanio na mambo yaliyozuliwa.

Sunan ni wingi wa Sunnah. Ni njia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Jilazimieni na Sunnah zangu… “

Bi maana njia yangu.

Kwa mujibu wa wanazuoni wa Hadiyth na elimu ya istilahi Sunnah maana yake ni yale yaliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ni mamoja iwe ni maneno, matendo, kulikubali jambo au sifa. Maana maalum ni ule upambanuzi wa wanazuoni wa Hadiyth.

Hapa tunajifunza ya kwamba ni lazima kutumia Sunnah kama dalili baada ya Qur-aan. Sunnah ni chanzo cha pili miongoni mwa vyanzo vya Uislamu baada ya Qur-aan tukufu.

Misingi ya kujengea dalili kwa mujibu wa wanazuoni kuna ambayo kuna maafikiano juu yake na kuna mingine ambayo kuna tofauti juu yake. Misingi ambayo kuna maafikiano juu yake ni ifuatayo:

1 – Msingi wa kwanza ni Qur-aan Tukufu.

2 – Msingi wa pili ni Sunnah ya Mtume. Kwa kuwa ni Wahy wa pili baada ya Qur-aan. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

“Yale anayokupeni Mtume yachukueni, na yale anayokukatazeni yaacheni.” (59:07)

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kupata fitina au ikawasibu adhabu iumizayo.” (24:63)

Huu ndio msingi wa pili ambao ni Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa sababu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kama Mola alivyomsifu:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

“Wala hatamki kwa matamanio. Hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.” (53:03-04)

Kwa ajili hii wanazuoni wanaita – Sunnah – kuwa ni Wahy wa pili baada ya Qur-aan tukufu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 58-59
  • Imechapishwa: 17/12/2023