10. Unataka kufaulu? – basi shikamana na mambo haya matatu

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

لعلك تُفلحُ

…huenda ukafaulu

Bi maana ikiwa unataka kufaulu ambako ni furaha katika maisha ya duniani na Aakhirah, basi shikamana na kamba ya Allaah na ufuate uongofu. Hii ndio njia ya furaha. Kufaulu maana yake ni kheri nyingi na kupata furaha. Amesema (Ta´ala):

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Hakika wamefaulu waumini ambao katika swalah zao wananyenyekea.” (23:01-02)

Mpaka alipofikia kusema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Na ambao wanazihifadhi swalah zao – hao ndio warithi ambao watarithi [mabustani ya] al-Firdaws wao humo ni wenye kudumu.” (23:09-11)

Hizi ndio sababu za kufaulu. Ikiwa unataka kufaulu basi ni lazima kwako ushikamane na mambo haya matatu:

1 – Shikamana na kamba ya Allaah.

2 – Ufuate uongofu.

3 – Jiepushe na Bid´ah.

Ukikosa moja katika mambo haya matatu basi utakhasirika na hutofaulu kamwe. Amesema (Ta´ala):

فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ

“Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, hao ndio wenye kufaulu; na yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu, basi hao ni wale ambao wamekhasirika nafsi zao Motoni watakuwa ni wenye kudumu.” (23:102-103)

Hiki ndiko kinyume cha kufaulu: ni khasara. Si kwamba wamekhasirika mali zao. Bali wamekhasirika nafsi zao. Mtu kukhasirika nafsi yake ndio khasara kubwa kabisa. Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ

“Sema: “Hakika waliokhasirika ni wale waliokhasiri nafsi zao na familia zao Siku ya Qiyaamah.” Tanabahi!  Huko ndiko kukhasirika kwa wazi.” (39:15)

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaa):

“… huenda…”

Haya ni matarajio. Kwa sababu ´Aqiydah sahihi ni kwamba hatumkatii yeyote kufaulu isipokuwa yule aliyekatiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au ikatajwa ndani ya Qur-aan ya kwamba mtu huyo amefaulu. Yule ambaye hakutajwa si katika Qur-aan wala Sunnah kwa dhati yake ya kwamba ni katika waliofaulu sisi hatumthibitishii kufaulu. Lakini hata hivyo tunatarajia wema kwa walio wema na tunachelea kwa wenye kutenda mabaya. Sababu nyingine ni kuwa muislamu asighurike na matendo yake. Maana ya maneno yake:

“… huenda ukafaulu.”

Bi maana usighurike na matendo yako. Lakini hata hivyo jibidishe matendo mema na utaraji kuwa Allaah atakujaalia kuwa miongoni mwa wenye kufaulu. Usitegemee kufaulu pake yake pasi na matendo. Huu ni mwenendo wa wapotevu. Haya ndio matarajio yenye kusimangwa. Matarajio yenye kusifiwa ni yale yenye kuambatana na matendo mema. Kwanza fanya sababu kisha mtegemee Allaah (´Azza wa Jall).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 56-57
  • Imechapishwa: 17/12/2023