09. Radd kwa wenye kusema kuna Bid´ah nzuri

Kwa ufupi ni kwamba Bid´ah ni shari hata kama watu wake watadai kuwa ni kheri. Hata kama watasema kuwa Bid´ah imegawanyika sehemu mbili:

1- Bid´ah nzuri.

2 – Bid´ah mbaya.

Tunawaambia kuwa hakuna kitu kizuri katika Bid´ah kwenye dini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila Bid´ah ni upotevu.”

Yule mwenye kusema kuwa kuna Bid´ah nzuri basi huku ni kukadhibisha maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kila Bid´ah ni upotevu.”

na:

“Yeyote mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na dini yetu, atarudishiwa mwenyewe.”

Katika dini hakuna Bid´ah nzuri hata siku moja.

Kuhusu yale waliyodai kwamba ni Bid´ah nzuri ikiwa ni pamoja vilevile na ujenzi wa masomo, kutunga vitabu n.k., tunawaambia kuwa sio Bid´ah. Uhakika wa mambo ni kuwa dini imesisitiza katika mambo haya. Ni njia zinazopelekea katika mambo yaliyowekwa katika Shari´ah. Dini imesisitiza kutenda wema, matendo mema na kufanya mambo ya kheri. Zote hizi ni njia za kheri. Ni mambo yanasaidia katika kutenda kheri. Kwa hivyo sio Bid´ah. Mambo haya yameletwa na dini na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakokoteza kwayo. Amesema (Ta´ala):

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ

“Saidianeni katika wema na uchaji Allaah, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui.” (05:02)

Kuhusu maneno yake (´alayhis-Salaam):

“Ambaye ataweka katika Uislamu msingi mzuri basi atapata ujira wake na ujira wa yule atakayeufanya.”[1]

Kikusudiwacho ni mtu amehuisha Sunnah iliyofishwa na baadaye watu wakamfuata katika hilo. Mtu huyu atapata ujira wake na ujira wa atakayemuiga na kumfuata. Haina maana kwamba ni Bid´ah nzuri. Kinyume chake ni Sunnah.

Kufunza elimu yenye manufaa na kutendea kazi mambo yenye kumsaidia mtu na kujifunza elimu kama mfano wa kufungua masomo, kuanzisha vyuo vikuu na kufungua vituo vyenye kuwaunganisha wanafunzi. Yote haya ni katika mambo yenye kusaidia katika kujifunza elimu. Ni mambo yameamrishwa Kishari´ah na sio Bid´ah.

Kuhusu kuzua katika mambo yasiyohusiana na dini, kwa mfano kuvumbua mambo ya viwanda, ndege, gari na vyombo vya bahari. Hayahusiani na dini. Ni mambo yameruhusiwa. Sio kuzua katika dini. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَسَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مِّنْهُ

“Amekutiishieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini vyote humo.” (45:13)

Ni kwa ajili ya manufaa yenu nyinyi. Mambo haya hayaingii katika ´ibaadah. Hata hivyo vinaweza kumsaidia mtu kufanya ´ibaadah. Kwa mfano tunapanda gari kwa ajili ya kwenda hajj, kuwaunga ndugu, kufikia jambo la halali, kwa ajili ya kwenda kufanya biashara na pikniki. Yote haya ni katika mambo yenye manufaa ya mbinguni na ardhini ambayo Allaah ametuhalalishia. Hayana lolote kuhusiana na dini. Ni mambo ya kidesturi na yaliyoruhusiwa. Hatuyaiti kuwa ni Bid´ah. Isipokuwa ikiwa kama mtu anakusudia kwa upande wa lugha kwa kuwa ni mambo mepya ingawa yamejitokeza katika wakati fulani na hayakujitokeza hapo kabla. Watu wameyaweza ilihali hapo kabla watu walikuwa hawayawezi.

Ni wajibu kuyajua mambo haya. Kwa kuwa wapotevu wanataka kuwapaka watu mchanga wa machoni. Wanauliza: “Sasa mambo yote imekuwa ni Bid´ah?” Tunawaambia: sio kila kitu ni Bid´ah. Bid´ah ni yale yaliyozushwa katika dini ilihali hayapo na wakati huohuo yakawa hayana dalili si katika Qur-aan wala Sunnah. Mbali na hayo sio Bid´ah. Ni miongoni mwa mambo ambayo Allaah amewaruhusu waja Wake. Kuna tofauti kati ya hayo mawili.

[1] Muslim (69) na (1017)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 53-56
  • Imechapishwa: 17/12/2023