08. Maana ya Bid´ah kwa mujibu wa lugha na Shari´ah

Bid´ah kilugha maana yake ni kitu kilichozuliwa ambacho hakikutanguliwapo kuwa na mfano. Kwa mfano mtu anaweza kusema:

“Kitu hiki kimezuliwa.”

Bi maana kipya. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ

“Mwanzilishi wa mbingu na ardhi.” (02:117)

Bi maana Aliyevianzilisha bila ya kutanguliwapo kuwa na mfano wake. Kadhalika anasema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

قُلْ مَا كُنتُ بِدْعًا مِّنَ الرُّسُلِ

“Sema: “Mimi sikuwa jambo jipya lilozuka miongoni mwa Mitume.”” (46:09)

Bi maana mimi sio Mtume wa kwanza. Bali kabla yangu walikuwepo Mitume wengi. Mimi sio mzuka, yaani mpya ambaye hakukutangulia kuwepo mfano wangu katika nyumati zilizotangulia.  Ni vipi mtanikemea mimi kuwa Mtume wa Allaah ilihali kabla yangu kulikuwepo Mitume tu wengi?

Bid´ah Kishari´ah maana yake ni mambo yaliyozushwa katika dini yasiyokuwemo na wakati huohuo yakawa hayana dalili si katika Qur-aan wala Sunnah.

Bid´ah haina kheri yoyote. Inamtenga mtu mbali na Allaah na inamkasirisha Allaah (´Azza wa Jall). Kuhusu Sunnah yote ni kheri na Allaah anairidhia, anaipenda na kulipa thawabu kwayo. Kadhalika Allaah (Ta´ala) anaichukia Bid´ah, anawachukia Ahl-ul-Bid´ah na anaadhibu juu yake. Kwa hivyo hakuna nafasi yoyote ya kuongeza, kuweka mambo yenye kuonelewa kuwa ni mazuri na kuwafuata watu kwa yale waliyomo. Ni lazima kwanza kujua dalili zao. Endapo watakuwa katika haki, tutawafuata. Amesema (Ta´ala):

وَاتَّبَعْتُ مِلَّةَ آبَائِي إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ

“Nimefuata dini ya baba zangu; Ibraahiym, Ishaaq na Ya’quub.” (12:38)

Huku ni kufuata kwa haki. Lakini endapo watakuwa katika isiyokuwa haki hatuwafuati hata kama watakuwa ni watu bora kabisa.

Manaswara pindi walipozua utawa ambao Allaah hakuwaandikia walipotea kwa sababu hiyo. Isitoshe hawakuweza kuutekeleza. Uliwashinda kuutekeleza. Kwa sababu wao wenyewe ndio walijibebesha wasiyoyaweza. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) haikalifishi nafsi yoyote isipokuwa yale inayoyaweza. Lakini wao walijibebesha mambo wasiyoyaweza. Hatimaye utawa ukawashinda na wakauacha:

فَمَا رَعَوْهَا حَقَّ رِعَايَتِهَا

“Hawakuuchunga ipasavyo kuchungwa.” (57:27)

إِلَّا ابْتِغَاءَ رِضْوَانِ اللَّـهِ

“… isipokuwa ni kutafuta radhi za Allaah.” (57:27)

Ni jambo walizua wakitaka kupata radhi za Allaah. Hii ni dalili inayofahamisha kuwa kinachozingatiwa ni dalili. Lengo na nia peke yake havitoshelezi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 52-53
  • Imechapishwa: 17/12/2023