07. Dini imekamilika na hakuna haja ya nyongeza

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

ولا تكُ بدعيا لعلك تُفلحُ

usiwe mzushi huenda ukafaulu

MAELEZO

Haya ni makatazo. Huu ni unasibisho wa Bid´ah. Bid´ah ni kile kilichozuliwa katika dini ambacho hakina msingi si katika Qur-aan wala Sunnah. Allaah ametukataza kuzua katika dini. Vivyo hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametutahadharisha kuzua katika dini. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu Nimekutimizieni neema Yangu na Nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.” (05:03)

Dini imekamilika na haina haja ya kuiongezea mambo ambayo wewe unaonelea kuwa ni mazuri au ukawafuata kichwa mchunga wengine ilihali mambo hayo hayana dalili katika Qur-aan wala Sunnah ukajikurubisha kwayo kwa Allaah. Kwa mfano Adhkaar za Bid´ah, swalah za Bid´ah na aina nyenginezo zote za kujikurubisha kwa Allaah endapo yatakuwa hayana dalili. Katika hali hiyo itakuwa ni Bid´ah. Haijalishi kitu hata kama nia ya mwenye kufanya hivo ni nzuri anachokusudia ni kupata ujira na thawabu na hakusudii kwenda kinyume. Yeye ameonelea kuwa jambo hilo lina kheri na hivyo akalifanya kuwa zuri. Uhakika wa mambo jambo hilo halina kheri yoyote. Kama lingekuwa na kheri basi lingetajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah:

وَمَا كَانَ رَبُّكَ نَسِيًّا

“Mola wako si Mwenye kusahau kabisa.” (19:64)

مَّا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِن شَيْءٍ

“Hatukupuuza katika Kitabu kitu chochote.” (06:38)

Kheri zote na uongofu unapatikana katika Qur-aan na Sunnah. Ambaye ataleta nyongeza isiyokuwepo katika Qur-aan na Sunnah, basi hiyo ni Bid´ah yenye kurudishwa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na dini yetu, atarudishiwa mwenyewe.”[1]

“Yeyote mwenye kuzua katika dini yetu hii yale yasiyokuwemo, atarudishiwa mwenyewe.”[2]

Haijuzu kuzua katika dini au kufanya kitu ambacho hakuja nacho Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mtu akawa ni mwenye kujikurubisha kwacho mbele ya Allaah. Hii ni Bid´ah. Kila Bid´ah ni upotevu.

[1] Muslim (18) na (1718)

[2] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (18) na (1718)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 51-52
  • Imechapishwa: 17/12/2023