Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

واتبعِ الهُدى

… na ufuate uongofu

Uongofu ni dini aliyotumilizwa nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ

“Yeye ndiye ambaye amemtuma Mtume Wake kwa uongofu na dini ya haki ili ishinde juu ya dini zote japo watachukia washirikina.” (09:33)

Uongofu kwa maana nyingine ni elimu yenye manufaa. Dini ya haki ni yale matendo mema. Tunasoma mwishoni mwa “al-Faatihah”:

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ

“Tuongoze njia iliyonyooka. Njia ya wale Uliowaneemesha, sio ya walioghadhibikiwa wala waliopotea.” (01:06-07)

Ambao Allaah amewaneemesha ni wale waliokusanya kati ya elimu yenye manufaa na matendo mema. Walioghadhibikiwa ni wale waliojifunza elimu na wakaacha kutenda. Waliopotea ni wale walioenda kutenda pasi na kuwa na elimu. Mfano wa watu hawa ni kama wale Suufiyyah na wafanya ´ibaadah wajinga.

Kuna sampuli mbili za uongofu[1]:

1 – Uongofu wenye maana ya kuelekeza na kuibainisha haki. Huu ni ule uongofu ulioenea. Allaah amewaongoza watu wote kwa maana ya kwamba amewabainishia haki. Amesema (Ta´ala):

وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ عَلَى الْهُدَىٰ

“Ama kina Thamuud Tuliwaongoza, lakini hata hivyo walifadhilisha upofu juu ya uongofu.” (41:17)

Huu ni uongofu wa maelekezo.

2 – Uongofu wa kuongozwa kuitendea kazi haki na kushikamana nayo. Uongofu huu ni maalum na hauwi isipokuwa kwa watu walio na imani. Hakuna mwenye kuumiliki isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna anayemiliki suala la kuiongoza mioyo isipokuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Amesema (Ta´ala):

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۚ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ

“Hakika wewe humwongozi umpendaye, lakini Allaah ndiye anamwongoza amtakaye; Naye anawajua zaidi waongokao.” (28:56)

Aina ya uongofu wa kwanza unamilikiwa na Mitume, Manabii na wanazuoni. Wote wanaelekeza, kubainisha na kuifahamisha haki. Kwa ajili hii amesema (Ta´ala) kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

“Bila shaka unaongoza kuelekea njia iliyonyooka.” (42:52)

Huenda mtu akauliza ni kwa nini Allaah (Jalla wa ´Alaa) amemwambia Mtume Wake katika Aayah:

وَإِنَّكَ لَتَهْدِي

“Bila shaka unaongoza… “

ilihali katika Aayah nyingine amesema:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ

“Hakika wewe huwezi humwongozi umpendaye.”

Kuna mgongano? Jibu ni hapana. Aayah inayosema:

وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

“Bila shaka unaongoza kuelekea njia iliyonyooka.”

bi manaa unaelekeza. Ama kuhusu Aayah inayosema:

إِنَّكَ لَا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ

“Hakika wewe huwezi humwongozi umpendaye.”

bi manaa huwezi kumuwafikisha mtu akaikubali haki. Hakuna mwenye uwezo wa jambo hilo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna mgongano kati ya Aayah mbili hizo. Ambaye anaweza kuona kuwa kuna mgongano ni yule ambaye hana elimu. Kuhusu yule ambaye yuko na ujuzi wa Qur-aan na elimu hakuna mgongano uliyopo katika Qur-aan na Sunnah. Qur-aan kamwe haiwezi kujigonga. Kadhalika Sunnah. Kwa sababu ni Uteremsho wenye kutoka kwa Mwingi wa hekima, Anayestahiki kuhimidiwa. Lakini hili linahitajia kwa yule mwenye uelewa na mwenye kuoanisha baina ya dalili.

[1] Tazama “Shifaa´-ul-´Aliyl”, uk. 65 ya Ibn-ul-Qayyim.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 50-51
  • Imechapishwa: 17/12/2023