05. Allaah ametahadharisha mifarakano na tofauti

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametahadharisha yale waliyotumbukiaemo nyumati zilizotangulia pindi zilipofarikiana. Amesema (Ta´ala):

وَمَا تَفَرَّقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَةُ

“Hawakufarikiana wale waliopewa Kitabu isipokuwa baada ya kuwajia hoja zinazobainisha.” (98:04)

Hawana udhuru wowote kwa sababu Allaah amewabainishia. Lakini hata hivyo wakaacha ubainifu huu na hatimaye wakafarikiana. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ ۚوَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

“Msiwe kama wale waliofarikiana na wakatofautiana baada ya kuwajia hoja zinazobainisha. Hakika hao watapata adhabu kuu.” (03:105)

فَبَعَثَ اللَّـهُ النَّبِيِّينَ مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ وَأَنزَلَ مَعَهُمُ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِيَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ فِيمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ ۚ وَمَا اخْتَلَفَ فِيهِ إِلَّا الَّذِينَ أُوتُوهُ مِن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ ۖ فَهَدَى اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا لِمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بِإِذْنِهِ ۗ وَاللَّـهُ يَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

“Allaah akatuma Manabii hali ya kuwa ni wabashiriaji na waonyaji na akateremsha pamoja nao Kitabu kwa haki ili kihukumu baina ya watu katika waliyokhitilafiana kwayo. Hawakukhitilafiana katika hayo isipokuwa wale waliopewa hicho Kitabu baada ya kuwajia hoja zinazobainisha kwa uhusuda kati yao. Allaah akawaongoza wale walioamini kuendea haki katika yale waliyokhitilafiana kwa idhini Yake. Hakika Allaah humwongoza amtakaye kuelekea njia iliyonyooka. (02:213)

Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alikuwa anasimama kuswali usiku alikuwa akisema:

اللَّهُمَّ رَبَّ جِبْرِيلَ وَمِيكَالَ وَإِسْرَافِيلَ فَاطِرَ السَّمَواتِ والأَرْضِ عَالِمَ الْغَيْبِ والشَّهَادَةِ أَنْتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادك فِيما كانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ اهْدِنِي لِمَا اخْتُلِفَ فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بإِذْنِكَ إِنَّكَ تَهْدِي مَنْ تَشَاءُ إِلى صِرَاطٍ مُسْتَقِيم

“Ee Allaah! Mola wa Jibraaiyl, Mikaa-il na Israafiyl! Mwenye kuziendesha mbingu na ardhi, mjuzi wa vilivyodhahiri na viliyojificha. Hakika wewe utahukumu kati ya waja Wako katika yale waliyokuwa wakitofautiana kwayo. Niongoze katika haki kwa yale kumetokea tofauti kwayo, kwani hakika Wewe unamwongoza umtakaye katika njia iliyonyooka.”[1]

Hii ni du´aa tukufu ambayo Allaah anamkinga kwayo muislamu kutokamana na matamanio, mitihani na shari.

[1] Muslim (200) na (770)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 48-49
  • Imechapishwa: 16/12/2023