Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ukiambiwa: “Ni misingi ipi mitatu ambayo ni wajibu kwa mtu kuijua?” sema: “Mja kumjua Mola Wake, Dini yake na Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Kukisemwa: “Ni nani Mola Wako?” Jibu: “Mola Wangu ni Allaah ambaye Amenilea na Akawalea walimwengu wote kwa neema Zake. Yeye ndiye ninayemwabudu na sina mwabudiwa mwingine asiyekuwa Yeye.” Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

Sifa njema zote ni za Allaah, Mola wa walimwengu.” (al-Faatihah 01 : 02)

Kila kisichokuwa Allaah ni walimwengu [kimeumbwa] na mimi ni mmoja katika walimwengu hao.

MAELEZO

Misingi hii mitatu imekusanya dini yote; ni nani Mola Wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume Wako? Mja huulizwa maswali haya matatu ndani ya kaburi lake.

Ukiulizwa: “Ni nani Mola Wako?”, sema: “Mola wangu ni Allaah aliyenilea na akawalea walimwengu wote kwa neema Zake. Yeye ndiye ninayemuabudu na sina mwengine ninayemuabudu asiyekuwa Yeye. Huyu ndiye Mola wa wote. Allaah (Ta´ala) amesema:

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Sifa njema zote ni za Allaah, Mola wa walimwengu.” (01:02)

Majini, watu, wanyama, milima na miti vyote ni katika walimwengu. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi. Anafunika usiku kwa mchana, unaufuatia upesi upesi na [ameumba] jua na mwezi na nyota vimetiishwa kwa amri Yake. Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.” (07:54)

Yeye ndiye Mola wa wote. Uumbaji na amri vyote ni Vyake. Yeye pekee ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa. Kwa ajili hii amesema (Subhaanah):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Ambaye amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kucha.” (02:21)

Yeye ndiye ninayemuabudu na mimi sina ninayemuabudu mwengine asiyekuwa Yeye. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Sifa njema zote ni za Allaah, Mola wa walimwengu.” (01:02)

Bi maana sifa zote zinamstahikia Allaah. ´Ibaadah ni katika sifa na himdi.

Vyote visivyokuwa Allaah vimeumbwa. Majini, watu, wanyama na milima vyote vimeumbwa. Mimi ni mmoja wa walimwengu hao ambao Allaah amewaumba na akawafanya wapatikane. Amewawajibishia wamtii. Ni lazima kwa walimwengu wote katika majini na watu ambao wana majukumu juu ya matendo yao wamtii Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wamuabudu Yeye pekee. Hali kadhalika Malaika ni wajibu kwao kumuabudu Allaah pekee. Kwa ajili hii Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Malaika:

لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ

“Hawamuasi Allaah, kwa yale anayowaamrisha, na wanafanya yale wanayoamrishwa.” (66:06)

لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ وَهُم مِّنْ خَشْيَتِهِ مُشْفِقُونَ

”Hawamtangulii kwa maneno, nao kwa amri Yake wanatenda. Anayajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na wala hawataomba uombezi wowote isipokuwa kwa yule ambaye amemridhia, nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea.” (21:27-28)

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 04/12/2016