14. Hivi ndivyo utamtambua Mola Wako unayemuabudu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kukisemwa: “Vipi umemjua Mola Wako?” jibu: “Kwa alama Zake na viumbe Vyake. Miongoni mwa alama Zake ni usiku, mchana, jua na mwezi. Miongoni mwa viumbe Vyake ni mbingu saba na ardhi saba, vilivyomo ndani yake na vilivyomo kati yake.” Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ

”Na katika alama Zake ni usiku na mchana, jua na mwezi. Hivyo basi msisujudie jua na wala mwezi,
bali msujudieni Allaah Ambaye Aliyeviumba – ikiwa Yeye Pekee ndiye mnamwabudu.” 
(Fuswswilat 41 : 37)

Vile vile Amesema (Ta´ala):

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi. Anafunika usiku kwa mchana, unaufuatia upesi upesi na [ameumba] jua na mwezi na nyota vimetiishwa kwa amri Yake. Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.” (07:54)

Mola ndiye Mwabudiwa. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Ambae Amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na ucha Mungu. Ambaye Amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa na Akateremsha kutoka mbinguni maji, Akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Hivyo basi msimfanyie Allaah washirika na hali ya kuwa nyinyi mnajua.” (al-Baqarah 02 : 21-22)

Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Muumbaji wa vitu hivi ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa.”

MAELEZO

Mwandishi (Rahimahu Allaah) anamaanisha iwapo wewe, muislamu, utaulizwa ni vipi umemjua Mola wako ambaye wewe unamuabudu, unatakiwa kusema kuwa umemtambua kwa alama na viumbe Wake. Bi maana umemtambua kwa alama Zake nyingi na kwa viumbe Vyake vikubwa ambavyo vinavyothibitisha kuwa Yeye ni Mola mkubwa na kwamba Yeye ni Muumbaji mjuzi ambaye anastahiki kuabudiwa. Vyote hivyo vinafahamisha kuwa Yeye anaumba anavyovitaka, anatoa na kuzuia, ananufaisha na kudhuru. Katika mikono Yake kuna kila kitu (Subhaanahu wa Ta´ala).

Yeye ndiye mwenye haki ya kuabudiwa kwa kutiiwa, kuombwa, kutakwa uokozi na matendo yetu mengine yote tunayofanya. Kwa kuwa Allaah ndiye katuumba. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na wanaadamu isipokuwa waniabudu.” (51:56)

´Ibaadah inahusiana na kumpwekesha na kumtii Yeye pekee, kufuata Shari´ah Yake na kuyaadhimisha maamrisho na makatazo Yake kwa maneno na kwa vitendo.

Dalili ya kumtambua Allaah kupitia alama Zake ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ

”Miongoni mwa alama Zake ni usiku na mchana na jua na mwezi. Msisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Allaah aliyeviumba ikiwa Yeye pekee mnawambudu.” (41:37)

Yote haya yanafahamisha kuwa Yeye ndiye Mola wa walimwengu na ndiye Muumbaji mjuzi. Analeta usiku kwa viza vyake na anaufanya usiku kwenda kwa mwanga wake; pindi mchana unakuja usiku unapotea. Jua hili linawaangazia watu wote ulimwenguni. Kila mmoja ananufaika nalo. Hali kadhalika inahusiana na mwezi wakati wa usiku. Hizi ni katika alama za Allaah kubwa. Vivyo hivyo ardhi na milima, mito, bahari, miti na wanyama vilivyomo ndani yake. Vilevile mbingu ambayo watu wanaiona ni katika alama za Allaah zinazofahamisha ukubwa Wake na kwamba Yeye ni Mola wa walimwengu na kwamba ni Muumbaji mjuzi ambaye anastahiki kuabudiwa. Kwa ajili hiyo amesema:

وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ

”Miongoni mwa alama Zake ni usiku na mchana na jua na mwezi. Msisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Allaah aliyeviumba ikiwa Yeye pekee mnawambudu.” (41:37)

Bi maana usiviabudu viumbe hivi. Muabudu aliyeviumba na kufanya vipatikane ambaye ni Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Yeye ndiye anayestahiki mja kumdhalilikia na kumnyenyekea. Maamrisho Yake yanatakiwa kutekelezwa na makatazo Yake kuepukwa. Yote hayo yafanyike kwa maadhimisho, matakaso, kuogopa adhabu Zake na kuwa na shauku juu ya thawabu Zake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 22-24
  • Imechapishwa: 04/12/2016