Allaah (Ta´ala) amesema:

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah.” 14:27

Wafasiri wengi wa Qur-aan wanasema kuwa ni neno la Tawhiyd ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah katika uhai wa dunia, yaani kabla ya kufa, na Aakhirah, yaani ndani ya kaburi. Wanachuoni wengine wanasema kuwa katika uhai wa dunia hii ni ndani ya kaburi na mitihani yake na Aakhirah ni siku ya Qiyaamah. Hata hivyo maoni ya kwanza ndio sahihi zaidi.

al-Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi muislamu anapohojiwa ndani ya kaburi lake na akashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ndiye Mtume Wake hiyo ndio tafsiri ya maneno ya Allaah (Ta´ala):

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah.” 14:27

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Imeteremshwa juu ya adhabu ya kaburi. Ataambiwa: “Mola wako ni nani?” Atasema: “Mola wangu ni Allaah na Mtume wangu ni Muhammad.” Hiyo ndio tafsiri ya maneno ya Allaah (Ta´ala):

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah.” 14:27

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Imaam Ahmad ameipokea kwa muundo mrefu na kadhalika imepokelewa katika Sunan na Musaaniyd.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi mmoja wenu anapokufa huonyeshwa mahala pake asubuhi na jioni. Akiwa ni katika watu wa Peponi, ni katika watu wa Peponi. Akiwa ni katika watu wa Motoni, ni katika watu wa Motoni. Ataambiwa: “Hapa ndipo mahala pako mpaka hapo Allaah atapokufufua siku ya Qiyaamah.”

Ameipokea vilevile Imaam Ahmad katika “al-Musnad” yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 196
  • Imechapishwa: 03/12/2016