5 – Kuamini Hodhi ya Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika uwanja wa Qiyaamah. Hodhi hiyo, kama ilivyoelezwa katika Hadiyth mbalimbali, ni Hodhi itayokuwepo siku ya Qiyaamah ambayo inamimina humo maji kutoka katika mto wa al-Kawthar Peponi. Maji yake ni meupe mno kuliko maziwa, matamu zaidi kuliko asali na yenye baridi zaidi kuliko theluji. Urefu wake ni mwendo wa mwezi, upana wake ni mwendo wa mwezi na vikombo vyake ni sawa na idadi ya nyota mbinguni. Ambaye atakunywa humo basi hatohisi tena kiu mpaka atakapoingia Peponi. Imethibiti katika Hadiyth ya kwamba kuna watu watakaofukuzwa mbali nayo ambao wamebadilisha na kugeuza kama anavyofukuzwa ngamia mwenye kiu ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aseme:

“Watokomee mbali wale waliobadilisha baada yangu.”[1]

6 – Kuamini Njia. Ni Njia yenye kuhisiwa itayowekwa juu ya daraja la Moto wa Jahannam. Watu watapita juu yake kutegemea matendo yao. Wako watu ambao watapita juu yake kama umeme, wengine kama upepo, wengine kama ndege, wengine kama farasi endae mbio, wengine watakimbia, wengine watatembea kwa miguu yao na wako wengine watatambaa. Juu ya Njia hiyo kutakuwepo ndoano inayomvuta aliyeamrishwa kumvuta. Mwenye kuokoka amesalimika na atakayevutwa atatumbukia kifudifudi ndani ya Motoni. Ambaye atavuka na kuipita daraja basi ameokoka na atakuwa miongoni mwa watu wa Peponi[2]. Amesema (Ta´ala):

وَإِن مِّنكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا ۚ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ حَتْمًا مَّقْضِيًّا ثُمَّ نُنَجِّي الَّذِينَ اتَّقَوا وَّنَذَرُ الظَّالِمِينَ فِيهَا جِثِيًّا

“Na hakuna yeyote miongoni mwenu isipokuwa ataufikia. Hiyo kwa Mola wako ni hukumu ya lazima kutimizwa. Kisha tutawaokoa wale waliomcha Allaah na tutawaacha madhalimu humo wamepiga magoti.”[3]

7 – Kuamini Pepo na Moto na kwamba ni makazi mawili ya malipo ya matendo. Pepo ni makazi ya waumini na wenye kumwabudu Allaah pekee. Moto ni makazi ya makafiri na watenda maovu wakiwemo mayahudi, wakristo, wanafiki, wakanamungu na washirikina. Makafiri hawatofanyiwa hesabu kwa njia ya kupimwa mema na maovu yao kwa sababu wao hawana mema. Bali yatadhibitiwa kwayo na kuwafanya wayakubali kisha baada ya hapo watupwe Motoni. Allaah (Ta´ala):

يَوْمَ نَحْشُرُ الْمُتَّقِينَ إِلَى الرَّحْمَـٰنِ وَفْدًا وَنَسُوقُ الْمُجْرِمِينَ إِلَىٰ جَهَنَّمَ وِرْدًا

“Siku Tutakayowakusanya wenye kumcha Allaah kwenda kwa Mwingi wa rehema hali ya kuwa [juu ya vipando] kama ni wawakilishi wa heshima na tutawaendesha wahalifu kuelekea Motoni hali ya kuwa na kiu.”[4]

إِنَّ الْأَبْرَارَ لَفِي نَعِيمٍ وَإِنَّ الْفُجَّارَ لَفِي جَحِيمٍ

“Hakika waumini watendao mema kwa wingi bila shaka watakuwa katika neema na hakika watendao dhambi bila shaka watakuwa katika Moto uwakao vikali mno.”[5]

فَأَمَّا الَّذِينَ شَقُوا فَفِي النَّارِ لَهُمْ فِيهَا زَفِيرٌ وَشَهِيقٌ

“Ama wale walio mashakani , basi watakuwa Motoni – kazi humo ni kupumua kwa mngurumo na kuvuta pumzi kwa mkoromo.”

mpaka aliposema:

وَأَمَّا الَّذِينَ سُعِدُوا فَفِي الْجَنَّةِ خَالِدِينَ فِيهَا مَا دَامَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ إِلَّا مَا شَاءَ رَبُّكَ ۖ عَطَاءً غَيْرَ مَجْذُوذٍ

“Ama wale walio furahani, basi watakuwa katika mabustani, ni wenye kudumu ndani yake zitakavyodumu mbingu na ardhi isipokuwa atakavyo Mola wako – ni hiba isiyokatizwa.”[6]

[1] al-Bukhaariy (6584) na Muslim (2291).

[2] al-Haakim (8749) amepokea mfano wake na akasema:

“Ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.”

adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[3] 19:71-72

[4] 19:85-86

[5] 82:13-14

[6]  11:106-108

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Iymaan – Haqiyqatuhu wa Nawaaqidhwuh, uk. 22
  • Imechapishwa: 25/04/2023