13. Kifunguzi cha pili cha swawm: tendo la ndoa

2 – Mwenye kumwingilia mke wake mchana wa Ramadhaan hali ya kuwa amefunga, basi swawm yake imeharibika. Hapa ni pale ambapo atakuwa amekusudia na anajua. Atalazimika kuilipa siku hiyo, kuleta tawbah ya kweli, kujutia na kujikwamua. Aidha atalazimika kutoa kafara; ambayo ni kuacha mtumwa huru, asipopata basi atafunga miezi miwili mfululizo, asipoweza basi atawalisha chakula masikini sitini. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia:

“Wakati tulipokuwa tumekaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja bwana mmoja akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimeangamia!” Akasema: “Una nini?”

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Ni kipi kilichokuangamiza?” Akajibu: “Nimemwingilia mke wangu ilihali nimefunga.”

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Nimemsibu mke wangu katika Ramadhaan.

Ndipo Mtume wa Allaah akasema: “Unaweza kupata mtumwa ukamwacha huru?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kupata chakula cha kuwalisha masikini sitini?” Akajibu: “Hapana.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyamaza. Tulipokuwa katika hali hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja na chombo kilicho na tende ambapo akauliza: “Yuko wapi muulizaji?” Akajibu: “Ni mimi hapa.” Akamwambia: “Chukua ukatoe swadaqah.” Akasema: “Hivi kuna ambaye ni fakiri kuliko mimi, ee Mtume wa Allaah? Ninaapa kwa Allaah hakuna kati ya milima miwili hii watu wa nyumba ambao ni mafukara kuliko watu wa nyumbani kwangu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka yakaonekana magego yake. Kisha akasema: “Walishe watu wa nyumbani kwako.”[1]

Hadiyth inafahamisha kuwa mfungaji, ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia, mkazi, mzima, mwenye kukusudia na mwenye kukumbuka kufanya jimaa mchana wa Ramadhaan ni dhambi kubwa miongoni mwa madhambi makubwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumkubalia maneno yake aliposema:

“Nimeangamia.”

Imekuja pia katika Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyoipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake:

“Nimechomeka.”[2]

Lakini akifanya jimaa kwa kusahau basi swawm yake ni sahihi kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Hatolipa wala hatotoa kafara.

[1] al-Bukhaariy (1936) na Muslim (1111).

[2] Muslim (1112).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 18/04/2023