58 – Muhammad bin ´Abdillaah bin al-Mubaarak ametukhabarisha: Abu Daawuud ametukhabarisha, kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa ´Umar bin Sa´iyd, kutoka kwa Ibn Abiy Mulaykah, kutoka kwa ´Uqbah bin al-Haarith, ambaye amesimulia:

”Nilikuwa na Abu Bakr wakati alipopita karibu na al-Hasan. Abu Bakr akambeba juu ya mabega yake na kusema: ”Nimtoe fidia baba yangu kwako! Anafanana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na si ´Aliy.” ´Aliy alikuwa pamoja naye na akaanza kulia.”[1]

59 – ´Amr bin ´Aliy ametukhabarisha: Yahyaa ametukhabarisha: Ismaa´iyl ametukhabarisha: Abu Juhayfah ametukhabarisha:

”Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). al-Hasan bin ´Aliy alikuwa akifanana naye.”

60 – ´Aliy bin al-Husayn ametukhabarisha: Umayyah bin Khaalid ametukhabarisha: Shu´bah ametukhabarisha, kutoka kwa ´Adiy bin Thaabit, kutoka kwa al-Baraa’ bin ´Aazib, aliyesema:

”Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akimbeba al-Hasan juu ya mabega yake na kusema: ’”Ee Allaah! Hakika mimi nampenda huyu, basi Nawe mpende.”[2]

61 – al-Hasan bin Hurayth ametukhabarisha: Sufyaan ametukhabarisha, kutoka kwa ´Ubaydullaah bin Abiy Yaziyd, kutoka kwa Naafiy´ bin Jubayr, kutoka kwa Abu Hurayrah, ambaye amesimulia:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia al-Hasan: ”Ee Allaah! Hakika mimi nampenda basi Nawe mpende.”[3]

62 – Ismaa´iyl bin Mas´uud ametukhabarisha: Khaalid bin al-Haarith ametukhabarisha, kutoka kwa Ash´ath, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa mmoja katika Maswahabah zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – yaani Anas – ambaye amesema:

”Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitoa Khutbah na al-Hasan akiwa juu ya paja lake. Akizungumza kile anachotaka kuzungumza, akimwelekea, akimbusu na kusema: ’’Ee Allaah! Hakika mimi nampenda basi Nawe mpende.” Amesema pia: ”Mimi nataraji atakuja kusuluhisha kati ya makundi mawili ya ummah wangu.”[4]

63 – ´Abdullaah bin Sa´iyd ametukhabarisha: Sufyaan ametukhabarisha, kutoka kwa Abu Muusa, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa Abu Bakrah, aliyesema:

”Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akimkumbatia al-Hasan na kusema: ”Hakika mwanangu huyu ni bwana. Pengine Allaah atakuja kusuluhisha kupitia yeye kati ya makundi mawili ya waislamu.”

64 – Muhammad bin ´Abdil-A´laa ametukhabarisha: Khaalid ametukhabarisha: Ash´ath ametukhabarisha, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa mmoja katika Maswahabah zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – yaani Anas – ambaye amesema:

”Niliingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuona al-Hasan na al-Husayn wakizunguka juu ya tumbo lake. Akisema: ”Mtoto wangu kutoka katika ummah wangu.”[5]

65 – ´Amr bin Mansuur ametukhabarisha: Abu Nu´aym ametuhadithia: Sufyaan ametukhabarisha, kutoka kwa Abul-Jihaaf, kutoka kwa Abu Haazim, kutoka kwa Abu Hurayrah, ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule anayewapenda basi amenipenda na yule mwenye kuwachukia basi amenichukia.”[6]

Bi maana al-Hasan na al-Husayn.

66 – Muhammad bin Aadam bin Sulaymaan ametukhabarisha, kutoka kwa Marwaan, kutoka kwa al-Hakam – Ibn Abiy Nu´aym bin ´Abdir-Rahmaan – kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Abu Sa´iyd, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”al-Hasan na al-Husayn ni mabwana wa vijana wa watu wa Peponi isipokuwa tu ´Iysaa bin Maryam na Yahyaa bin Zakariyyaa.”[7]

67 – al-Hasan bin Ishaaq ametukhabarisha: ´Ubaydullaah ametuhadithia: ´Aliy bin Swaalih ametukhabarisha, kutoka kwa ´Aaswim, kutoka kwa Zirr, kutoka kwa ´Abdullaah, aliyehadithia:

”Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anaswali na kusujudu, al-Hasan na al-Husayn wakaanza kumpandia mgongoni mwake. Anapotaka mtu kuwazuia, anaashiria kwamba awaache. Alipomaliza kuswali akawaweka juu ya mapaja yake na kusema: ”Yule mwenye kunipenda basi awapende wawili hawa.”[8]

68 – ´Ubaydullaah bin Sa´iyd ametukhabarisha: Yahyaa ametukhabarisha, kutoka kwa at-Taymiy… Na al-Hasan bin Qaza´ah ametukhabarisha, kutoka kwa Sufyaan bin Habiyb: at-Taymiy ametukhabarisha, kutoka kwa Abu ´Uthmaan, kutoka kwa Usaamah bin Zayd, aliyesema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akinishika mimi na al-Hasan bin ´Aliy na kusema: ”Ee Allaah! Wapende, kwani hakika mimi nawapenda.”[9]

[1] al-Bukhaariy (3750 na 3542).

[2] al-Bukhaariy (3749).

[3] Muslim (2421).

[4] al-Bukhaariy (3746).

[5] al-Bukhaariy (3753).

[6] Ibn Maajah (142) na al-Haakim (3/166 na 171), ambaye amesema kuwa Hadiyth ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (117).

[7] at-Tirmidhiy (3768). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (3181).

[8] Ibn Hibbaan (6970). Cheni yake ya wapokezi ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swifatu Swalaat-in-Nabiy”, uk. 148.

[9] al-Bukhaariy (3747).

  • Muhusika: Imaam Ahmad bin Shu´ayb an-Nasaa’iy (afk. 303)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-us-Swahaabah, uk. 60-64
  • Imechapishwa: 08/09/2026