13. Daraja ya tatu ya makadirio: Matakwa

Daraja ya tatu: Utashi. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amekitaka kila kilichopo au kisichokuwepo mbinguni au ardhini. Kilichopo kipo kwa kuwa Allaah (Ta´ala) ametaka kiwepo. Kisichokuwepo hakipo kwa kuwa Allaah (Ta´ala) ametaka kisiwepo. Haya yako dhahiri katika Qur-aan tukufu. Allaah (Ta´ala) amethibitisha matakwa Yake katika matendo Yake na katika matendo ya waja. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Hichi [Kitabu] si jengine isipokuwa ni ukumbusho kwa walimwengu – kwa yule anayetaka miongoni mwenu anyooke. Lakini hamtotaka isipokuwa atake Allaah, Mola wa walimwengu.”[1]

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ مَا فَعَلُوهُ

“Na lau Angetaka Mola wako wasingeliyafanya hayo.”[2]

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلَ الَّذِينَ مِن بَعْدِهِم مِّن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ

“Lau angelitaka Allaah wasingelipigana wale wa baada yao baada ya kuwajilia hoja za wazi.”[3]

Allaah (Ta´ala) amebainisha kuwa matendo ya waja yanapitika kwa matakwa Yake.

Kuhusu matendo Yake (Ta´ala), mara nyingi yametajwa:

وَلَوْ شِئْنَا لَآتَيْنَا كُلَّ نَفْسٍ هُدَاهَا

“Tungelitaka, Tungeliipa kila nafsi mwongozo wake.”[4]

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ لَجَعَلَ النَّاسَ أُمَّةً وَاحِدَةً

“Kama angetaka Mola wako bila shaka Angewafanya watu wote kuwa ni ummah mmoja.”[5]

Kuna Aayah nyingi zinazothibitisha matakwa katika matendo ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

Imani ya kuamini makadirio haitimii isipokuwa mpaka tuamini kuwa kila kilichopo na kisichokuwepo kinatokamana na matakwa ya Allaah. Hakuna kisichokuwepo isipokuwa Allaah (Ta´ala) ametaka kisiwepo. Na hakuna kilichopo isipokuwa Allaah (Ta´ala) ametaka kiwepo. Haiwezekani kukawepo kitu mbinguni wala ardhini isipokuwa kwa utashi wa Allaah (Ta´ala).

[1] 81:27-29

[2] 06:112

[3] 02:253

[4] 32:13

[5] 11:118

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Qadhwaa’ wal-Qadar, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (5/224-225)
  • Imechapishwa: 25/10/2016