123. Msingi mkubwa katika majina na sifa za Allaah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

´Aqiydah yenye kuenea juu ya mada hii ni kwamba Allaah anasifiwa kwa yale aliyojisifu Mwenyewe, yale aliyomsifu Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kwa yale aliyosifiwa na wale wa mwanzo waliotangulia. Kusifia hakutakiwi kuvuka Qur-aan na Hadiyth.

MAELEZO

Shaykh (Rahimahu Allaah) alipomaliza utangulizi, alihamia katika mwanzo wa jawabu la swali aliloulizwa, nalo ni ipi kauli kuhusu majina ya Allaah na sifa Zake zilizotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah. Akaweka msingi wa jawabu kwa kusema: Msingi katika jambo hili ni kwamba yale yaliyotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah ni haki kwa uhakika wake. Tunamthibitishia Allaah bila kupotosha, kukanusha, kufanya namna wala kulinganisha. Huu ndio msingi mkubwa katika mlango huu: yale yote yaliyotajwa ndani ya Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu majina ya Allaah na sifa Zake, basi sisi tunayathibitisha bila kuingiza mawazo na maono yetu. Hatuyapotoshi maneno ya Allaah kutoka sehemu zake wala hayakanushi majina na sifa za Allaah. Kisha pia hatufananishi majina ya Allaah na sifa Zake na majina ya viumbe wala sifa zao. Halafu akabainisha yale wanayoyasema Salaf wa ummah huu, nayo ni kwamba wao wanathibitisha yaliyotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah. Hawavuki Qur-aan na Sunnah katika majina na sifa za Allaah.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 208-209
  • Imechapishwa: 09/07/2026