12. Zawadi ya tatu: Kulingani kwa hekima

Kulingania kwa Allaah kunakuwa kwa hekima, kisha kwa maneno mazuri, kisha kwa kujadiliana kwa njia bora zaidi kwa ambaye si dhalimu, kisha kwa kujadiliana kwa njia isiyokuwa bora kwa ambaye ni dhalimu. Kwa hivyo ngazi ni nne. Allaah (Ta´ala) amesema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ ۖ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi. Hakika Mola wako Yeye anamjua zaidi aliyepotea njia Yake Naye anawajua zaidi waliongoka.”[1]

وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِلَّا الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ ۖ وَقُولُوا آمَنَّا بِالَّذِي أُنزِلَ إِلَيْنَا وَأُنزِلَ إِلَيْكُمْ وَإِلَـٰهُنَا وَإِلَـٰهُكُمْ وَاحِدٌ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ

“Na wala msijadiliane na Ahl-ul-Kitaab isipokuwa kwa yale ambayo ni mazuri zaidi; isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Na semeni: “Tumeyaamini ambayo yameteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwenu na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja pekee; nasi Kwake tunajisalimisha.”[2]

Hekima ni kule kukifanya kitu kwa uzuri kwa kuyateremsha mambo sehemu zake na kuyaweka mambo mahali pake stahiki. Sio katika hekima ukafanya haraka na ukawataka watu wabadilike mara moja kutoka katika hali waliyomo na kwenda katika hali ambayo walikuwa nayo Maswahabah. Mwenye kutaka hivo ni mpumbavu akilini mwake hali ya kuwa mbali na hekima. Hekima ya Allaah inakataa kupatikana kwa jambo hili. Linalofahamisha hilo ni kwamba Muhammad ambaye ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ndiye kateremkiwa na Qur-aan, Shari´ah ilimteremkia hatua kwa hatua mpaka ikatulia na kukamilika ndani ya nyoyo. Alifaradhishiwa swalah wakati wa safari ya mbinguni miaka mitatu kabla ya kuhama kwenda Madiynah. Kuna maoni mengine yanayosema kuwa ni mwaka mmoja na nusu. Yapo maoni mengine yanayosema ni miaka mitano. Kwa msemo mwingine ni kwamba wanazuoni wametofautiana juu ya hilo. Pamoja na hivyo haikufaradhishwa kwa hali yake tunayoona sasa. Mara ya kwanza ilipofaradhishwa ilikuwa Dhuhr, ´Aswr, ´Ishaa na Fajr ni Rak´ah mbili. Maghrib ilikuwa Rak´ah tatu ili iwe ni Witr ya mchana. Baada ya kuhajiri na baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitikiwa na miaka kumi na tatu huko Makkah ndipo ikazidishwa swalah ya mkazi na hivyo ikawa ni Rak´ah nne katika Dhuhr, ´Aswr na ´Ishaa. Swalah ya Fajr ilibaki kama ilivyo. Kwa sababu ni ndani yake kunarefushwa kisomo cha Qur-aan. Maghrib vilevile ikabaki Rak´ah tatu kwa sababu ni Witr ya mchana.

Zakaah ilifaradhishwa mwaka wa pili baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhajiri Madiynah. Vilevile kuna uwezekano kwamba ilifaradhishwa Makkah lakini haikupangiwa viwango vyake, uwajibu wake na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwaagiza wajumbe kuchukua zakaah isipokuwa katika mwaka wa tisa baada ya kuhajiri Madiynah. Kwa hivyo ukuaji wa zakaah ukawa katika hatua tatu: Makkah:

وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

“Toeni haki yake [zakaah] siku ya kuvunwa kwake.”[3]

Hakukubainishwa ambayo ni wajibu wala kiwango ambacho inalazimika wajibu hiyo. Jambo wakaachiwa watu. Katika mwaka wa pili baada ya kuhajiri Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Madiynah ndipo zakaah ikabainishwa kwa viwango vyake. Katika mwaka wa tisa baada ya kuhajiri Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa anawaagiza wajumbe kwa watu wa mifugo na wakulima wa matunda ili kuchukua zakaah.

Tafakari kuzichunga hali za watu wakati Allaah (´Azza wa Jall), ambaye ndiye mwadilifu zaidi ya wanaohukumu kuliko mahakimu wote, anapoweka Shari´ah.

Vivyo hivyo inapokuja katika kufunga ilienda hatua kwa hatua katika uwekwaji Shari´ah wake. Mwanzoni ilipofaradhishwa mtu alikuwa anapewa khiyari kati ya kufunga na kulisha chakula. Baadaye ikalazimika kufunga. Kulisha kukabaki kwa ambaye hawezi kufunga kwa njia endelevu.

[1] 16:125

[2] 29:46

[3] 06:141

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 17-19
  • Imechapishwa: 03/11/2021