Kuna kisomo maalum katika swalah ya Tahiyyat-ul-Masjid?

Swali: Je, kuna kisomo chochote maalum wakati wa kuswali swalah ya mamkuzi ya msikiti?

Jibu: Haina kisomo maalum. Bali ni kama swalah nyenginezo ambapo ataswali katika kila Rak´ah al-Faatihah na kile ambacho kitamkuia wepesi. Kilicho cha wajibu ni kusoma al-Faatihah peke yake kwa sababu ni nguzo ya swalah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hana swalah ambaye hakusoma ufunguzi wa Kitabu.”[1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Sunnah ni yeye aiswali pale tu anapoingia msikitini ijapo ni katika wakati wa makatazo kama vile baada ya swalah ya ´Aswr na baada ya swalah ya Fajr. Hilo ni kutokana na ueneaji wa Hadiyth zinazofahamisha juu usuniwaji wake. Jengine ni miongoni mwa zile swalah zinazoswaliwa kutokana na sababu fulani kama mfano wa swalah ya kupatwa kwa jua na Rak´ah mbili za Twawaaf. Swalah zinazotokana sababu zinafaa katika wakati wowote kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni.

[1] al-Bukhaariy (714) na Muslim (595).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/295)
  • Imechapishwa: 03/11/2021