11. Ni lazima kwa mlinganizi awe mwingi wa subira

Tunachotaka kusema ni kwamba ni lazima kila mlinganizi afikwe na maudhi. Lakini ni lazima kwake kusubiri. Kwa ajili hiyo Allaah (Ta´ala) alisema kumwambia Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ تَنزِيلًا

“Hakika Sisi Tumekuteremshia Qur-aan uteremsho wa hatua kwa hatua.”[1]

Kilichokuwa kinatarajiwa ni Allaah amwambie ashukuru neema Yake kwa kuteremshiwa Qur-aan hii. Lakini amemwambia:

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلَا تُطِعْ مِنْهُمْ آثِمًا أَوْ كَفُورًا

“Basi subiri hukumu ya Mola wako na wala usimtii katika wao atendaye dhambi au mwenye kukufuru.”[2]

Hapa kuna maashirio kwamba kila ambaye atasimama kwa Qur-aan hii basi ni lazima afikwe na mambo chungumzima ambayo yanahitaji afanye uvumilivu mkubwa.

Kwa hivyo ni lazima kwa mlinganizi awe mwingi wa subira na aendelee mpaka pale Allaah atakapomfungulia. Sio lazima kwamba Allaah amfungulie wakati wa uhai wake. Bali jambo muhimu zaidi ni ulinganizi wako ubaki kati ya watu hali ya kukubaliwa na kufuatwa. Muhimu sio yule mtu. Kilicho muhimu ni ule ulinganizi. Kwa hivyo kukibaki ulinganizi wake, ijapo ni baada ya kufa kwake, basi anakuwa bado yuko hai. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

أَوَمَن كَانَ مَيْتًا فَأَحْيَيْنَاهُ وَجَعَلْنَا لَهُ نُورًا يَمْشِي بِهِ فِي النَّاسِ كَمَن مَّثَلُهُ فِي الظُّلُمَاتِ لَيْسَ بِخَارِجٍ مِّنْهَا ۚ كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْكَافِرِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Je, aliyekuwa maiti kisha Tukamuhuisha na tukamjaalia nuru anatembea kwayo kati ya watu, ni sawa na yule ambaye yuko katika viza si mwenye kutoka humo? Hivyo ndivyo walivyopambiwa makafiri yale waliyokuwa wakiyatenda.”[3]

Ukweli wa mambo ni kwamba uhai wa mlinganizi maana yake sio kule kubaki roho yake ndani ya kiwiliwili chake peke yake. Bali pia kule kubaki maneno yake kati ya watu. Tazamaa kisa cha Abu Sufyaan pamoja na Hiraql ambaye alikuwa amesikia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekwishatoka. Alimwita Abu Sufyaan na akamuuliza juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yeye kama yeye, ulinganizi wake na Maswahabah zake. Wakati Abu Sufyaan alipomjibu yale aliyomuuliza Hiraql akamwambia:

“Ikiwa yale unayosema ni kweli basi atamiliki yale yaliyo chini ya miguu yangu hii.”[4]

 Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu! Ni nani anayefikiri kuwa mfalme mwenye nguvu anaweza kusema maneno kama haya juu ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Pamoja na haya hakukomboa kisiwa cha kiarabu kutokamana na utumwa wa shaytwaan na matamanio. Ni nani anayeweza kufikiri kuwa mfano wa mtu huyu anaweza kusema maneno kama haya? Kwa ajili hii wakati alipotoka Abu Sufyaan alisema kuwaambia watu wake:

“Hakika limekuwa kubwa jambo la Ibn Abiy Kabshah. Hakika anamwogopa mfalme wa watu wa manjano.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimiliki yaliyo chini ya miguu ya Hiraql kwa ulinganizi wake na si kwa utu wake. Ulinganizi wake ulifika katika ardhi hiyo na ikafutilia mbali masanamu, shirki na watu wake. Aidha yakamilikiwa na wale makhalifah waongofu baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yaliyamiliki kwa ulinganizi na Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa hivyo ni lazima kwa mlinganizi afanye subira na mwisho mwema utakuwa wake akiwa mkweli pamoja na Allaah. Ni mamoja katika uhai au baada ya kufa kwake:

إِنَّ الْأَرْضَ لِلَّـهِ يُورِثُهَا مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۖ وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ

“Hakika ardhi ni ya Allaah; humrithisha amtakaye katika waja Wake. Na mwisho mwema ni kwa wale wenye kumcha Allaah.”[5]

إِنَّهُ مَن يَتَّقِ وَيَصْبِرْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ

”Hakika mwenye kumcha Allaah na akasubiri, basi hakika Allaah hapotezi ujira wa watendao wema.”[6]

[1] 76:23

[2] 76:24

[3] 06:122

[4] al-Bukhaariy (07).

[5] 07:128

[6] 12:90

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 03/11/2021